Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Utatuzi wa Migogoro ya Kisheria ni Jukumu la Pamoja - Maswi

Imewekwa: 30 Oct, 2024
Utatuzi wa Migogoro ya Kisheria ni Jukumu la Pamoja - Maswi

Na Lusajo Mwakabuku – WyKS Iringa

Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imekusudia kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutekeleza kampeni ya huduma za msaada wa kisheria bure kwa wananchi iitwayo Mama Samia Legal Aid Campaign.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Chacha Maswi, ametangaza mpango huu tarehe 28 Oktoba 2024, katika kikao kazi kilichofanyika Mkoani Iringa kwa siku tatu ambacho kilihusisha Viongozi wa juu wa TLS na Wizara.

Kampeni hiyo inayotekelezwa katika Mikoa yote Nchi nzima inalenga kutoa elimu ya kisheria na msaada wa kisheria katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, matunzo ya watoto na usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala na masuala yanayohusiana na haki za binadamu kwa ujumla.

Bw. Maswi amesisitiza kwamba kutatua migogoro ya kisheria ni jukumu la pamoja la Watanzania wote, na kwamba ushirikiano huo ni muhimu katika kuwasaidia wananchi kupata haki zao. Na kwamba kila mtanzania mzalendo ana wajibu wa kulinda haki inayopelekea amani na utulivu nchini.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika Tarehe 28 Oktoba 2024 Mkoani Iringa, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, amesisitiza umuhimu wa TLS na Serikali kuwafikia wananchi wa pembezoni ambao hawawezi kumudu gharama za Mawakili katika masuala mbalimbali yanayohitaji msaada wa kisheria.

Lengo kuu la kampeni hiyo, inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini huku ikitarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wote, bila kujali hali zao za kiuchumi.