Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Viongozi wa Dini Mna Dhima Kubwa Katika Kuhakikisha Amani na Upendo Nchini – Kabudi

Imewekwa: 28 Sep, 2024
Viongozi wa Dini Mna Dhima Kubwa Katika Kuhakikisha Amani na Upendo Nchini – Kabudi

Na Lusajo Mwakabuku    - WyKS Dar es Salaam.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amesema viongozi wa dini nchini wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha upendo na amani vinatawala nchini kwa kupitia mafundisho yao huku akiwasisitiza viongozi hao kuhubiri maadili ambayo hivi sasa yanaporomoka kwa visingizio vya utandawazi na haki za binadamu.

Waziri Kabudi ameyasema hayo tarehe 27/09/2024 alipoalikwa kama Mgeni Rasmi katika Mkutano Mkuu wa 53 wa Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya   uliofanyika katika eneo la Kitongoji cha Kitonga, kata ya Msongola iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam.

Waziri Kabudi alianza kwa kutoa shukrani kwa mwenyeji wake Shekhe Khawanja Muzaffar Ahmad Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahamadiyya Tanzania kwa kumualika na kuimwagia sifa  taasisi ya kidini ya Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya Tanzania kuwa ni taasisi kongwe iliyofanya kazi kubwa za kidini toka ilivyosajiliwa mwaka 1934, (Takriban Miaka 90) ambapo moja wapo ya kazi hizo ni kutangaza uislam  na  kurahisisha waumini kuwa na uelewa wa dini wanayoiamini kwani ni Jumuiya ya Kwanza kuandika Quran tukufu katika lugha ya kiswahili.

Aidha Kabudi aliendelea kwa kuwaomba viongozi wa dini waliohudhuria Mkutano huo wakiwemo, Mashekhe, Makhalifa na Masharifu kuendelea kuhimiza upendo, mshikamano na kuheshimiana kama Taifa.

“Lazima tujue viongozi wa dini mnayo dhima kubwa kuhakikisha amani na upendo katika  Taifa letu, vinakuwa kipaumbele namba moja na hayo yote yanawezekana ikiwa watu wetu watazingatia maelekezo ya dini zetu hasa katika kuwatii viongozi wetu na kujua kuwa Mungu atawapokea wale wanaoamini na kigezo muhimu cha wewe kuwa miongoni mwa wenye kuamini ni kuwa na upendo”. Alisema Waziri Kabudi.

Akiongelea suala la utii na maadili, Kabudi alisema “Upendo utatujengea utii na heshima baina yetu lakini kwa Mwenyezi Mungu ameagiza tutii Mitume, Viongozi wetu na mkubwa kumheshimu mdogo na mdogo kumheshimu mkubwa. Wakati huu tunapoelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa niwasihi muwakumbushe waumini wenu kuongeza upendo na kuwaheshimu na kuwatii viongozi wetu wa ngazi zote. Tukifanya hivyo tutakuwa tunatimiza maamrisho ya Mwenyezi Mungu (Azza wa Jall) kwetu”.

Pia Kabudi akatumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi wa dini na watu wote wenye nafasi za kupaza sauti kuendelea kuhimiza watu kushiriki uchaguzi ili kupata viongozi watakaotuongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo huku akiwataka watanzania kujitokeza kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura, na kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi unaokuja wa Serikali za Mitaa.

Kabudi alihitimisha hotuba yake kwa kuwahakikishia watu waliojitokeza katika mkutano huo kuwa milango ya Wizara yake ipo wazi wakati wote na kuwakaribisha kwa masuala yoyote yanayohusu sheria na upatikanaji wa haki huku akiongeza kuwa hivi karibuni alizindua Kituo cha kisasa cha kupokea malalamiko yoyote yanayohusu rushwa kubwa na ndogo na suala lolote linalopelekea uvunjifu wa haki nchini  kwa kupiga simu kupitia namba 0262 160360.

Pia alimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia uanzishwaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign, ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya Msaada wa kisheria sura 21, lengo likiwa ni kuwasaidia watanzania wote wanaohitaji huduma za kisheria ila wanashindwa kuzifikia kwa sababu aidha, ya kipato au sababu nyinginezo na kwamba  huduma hizi ni bure kabisa.