WANAFUNZI UDOM WAPEWA MBINU ZA KUMALIZA MIGOGORO BILA MAHAKAMA
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameshiriki katika mafunzo ya Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Usuluhishi mkoani Dodoma.
Mafunzo hayo yaliongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan, ambapo pia aliambatana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Bi. Zeraphina Gotora pamoja na Afisa Sheria Bw. Marwa Mohere kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, katika Shule ya Sheria ya Chuo hicho.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mhe. Jaji Khalfan amesisitiza umuhimu wa kutumia mbinu za usuluhishi katika kutatua migogoro badala ya kutegemea mifumo ya kawaida ya mahakama.
Ameeleza kuwa njia hii husaidia kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani, kuokoa muda na gharama, pamoja na kudumisha mahusiano mema kati ya wahusika wa mgogoro.
Katika mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Bi. Zeraphina Gotora na Afisa Sheria Bw. Marwa Mohere wa Wizara ya Katiba na Sheria wameshiriki kutoa elimu juu ya mbinu mbalimbali za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, huku wakiwahamasisha wanafunzi kuwa mabalozi wa amani katika jamii kwa kuhimiza suluhu badala ya migogoro ya muda mrefu inayoweza kuacha chuki.
Aidha, wanafunzi walipata fursa ya kufahamu majukumu ya Wizara ya Katiba na Sheria katika kusimamia masuala ya kisera na maadili ya watatuzi wa migogoro kwa njia mbadala jambo linalolenga kuhakikisha haki inapatikana kwa njia ya haraka, nafuu na yenye tija kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mwanafunzi wa Shule ya Sheria UDOM, Leila Mohammed, amesema mafunzo hayo yamewajengea uelewa mpana kuhusu umuhimu wa usuluhishi na kuwapa mbinu za vitendo za kushughulikia migogoro katika jamii.
Ameongeza kuwa wamepokea elimu hiyo kwa hamasa kubwa na wako tayari kuitumia katika maisha yao ya kila siku pamoja na taaluma yao ya sheria.
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwemo kutoa elimu kwa umma, kuandaa mafunzo kwa wadau mbalimbali, na kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya usuluhishi nchini ili kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani na kuongeza upatikanaji wa haki kwa wakati