Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wananchi Lupila Waitwisha MSLAC Kero ya Wanyama Waharibifu

Imewekwa: 31 May, 2024
Wananchi Lupila Waitwisha MSLAC Kero ya Wanyama Waharibifu

William Mabusi – WKS Makete

Wananchi wa Kijiji cha Lupila katika Kata ya Lupila Wilayani Makete wameitwisha Timu inayotekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Wilayani humo kero ya wanyama nyani na ngedere ambao wamekuwa tishio kwa kuharibu mazao na kutishia amani.

Malalamiko hayo yametolewa na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo Mei 30, 2024 ikiwa ni katika kutekeleza kampeni hiyo.

Bw. Naftali Ilomo mkazi wa kijiji cha Lupila wa kitongoji cha Upakilwa akitoa kero yake amesema, “Serikali ifanye utaratibu wa kuwafukuza nyani na ngedere maana wamekuwa kero karibu kwenye vijiji vyote vya Wilaya ya Makete iwe mvua iwe kiangazi, Wazazi wamekuwa wakihatarisha usalama wa watoto kwa kuwaacha majumbani kwenda kuhamia nyani na ngedere.”

Kilio kama hicho kilitolewa na wakazi wa kijiji cha Masisiwe Kata ya Ukwama ambao wameomba Serikali iwakusanye na kuwapeleka wanyama hao kwenye hifadhi ama sivyo waruhusiwe kuwaua.

Akitoa mada ya wanyamapori na makatazo kwenye Hifadhi za Taifa na Mapori Tengefu Afisa Wanyamapori Bw. Francis Malembo kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori – TAWA amesema ni kinyume cha sheria kuuwa wanyamapori bila kibali, kwa kufanya hivyo ni kuingia kwenye mgogoro na Serikali na ndiyo umuhimu wa kampeni hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuepusha migogoro.

“Mnapobaini wanyamapori kwenye maeneo yemu toeni taarifa kwa viongozi ambao nao watatoa taarifa kwa Afisa Wanyamapori wa Wilaya ili hatua stahiki zichukuliwe.” Alisema Bw. Malembo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Bw. William Makufwe alikiri kuwepo kwa changamoto ya ngedere kwenye maeneo mengi Wilayani humo na kwamba unaandaliwa utaratibu wa kuwafukuza na pale ambapo watakuwa wamezidi upo utaratibu wa kuwauwa lakini kwa malekezo maalum kutoka mamlaka husika.

Akihitimisha mada yake Bw. Malembo aligusia makatazo kwenye hifadhi za Taifa kuwa ni pamoja na mwananchi haruhusiwi kuingia kwenye hifadhi bila kibali, hairuhusiwi kufanya shughuli yoyote ya kijamii kama kukata kuni, kuingiza mifugo, kulima au kuwinda bila kibali.