Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wananchi Makete Waifagilia MSLAC

Imewekwa: 04 Jun, 2024
Wananchi Makete Waifagilia MSLAC

William Mabusi – WKS Makete

Wananchi Wilayani Makete wamesema Kampeni ya Msaaada wa Kisheria ya Mama Samia imewapa elimu ya kutosha kuwaepusha na migororo, wakati huo huo imewasaidia pakubwa kutatua migogoro waliyokuwa nayo.

Wananchi hao wametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano ya hadhara ya kutekeleza Kampeni hiyo Wilayani humo.

Bw. Amos Tweve mkazi wa kijiji cha Nkenja Kata ya Kitulo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo Juni 04, 2024 amesema “mtafikiri mlinusa kijiji hiki kina shida fulani mkaona mpeleke watu wenye taaluma hii waje kufundisha hiki mlichofundisha, naombeni elimu hii muifikishe kwa wantanzania wengine.”

Katika mkutano huo Bw. Daudi Kinga alisema “nyie hamjui tu ila kwa elimu hii kuna migogoro mingi mmeitatua, Mungu awabariki sana, nawaomba wananchi wenzangu twende tutekeleze waliyotwambia wataalam.”

Katika hatua nyingine Bi. Rose Mbogela mkazi wa kijiji cha Matamba Kata ya Matamba kwenye mkutano wa kampeni hiyo uliofanyika Juni 3, 2024 anasema hakujua afanye nini baada ya mume wake kufariki na eneo aliloishi na mume wake kuvamiwa na mtu akidai ni mali yake. Kitu cha kusikitisha zaidi ni pale ambapo Baraza la Ardhi la Kata lilipotoa hukumu iliyomnyima haki Bi. Mbogela kitu ambacho ni kinyume na sheria kwani Mabaraza ya Ardhi ya Kata hayatakiwi kutoa hukumu baada ya marekebisho ya sheria mwaka 2021. Hukumu hiyo ilitupiliwa mbali na Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Makete mwaka jana. Baada ya hukumu hiyo kutupiliwa mbali bado Bi. Mbogela amekuwa akiishi kwa vitisho, Timu ya MSLAC imemhakikishia Bi. Mbogela kwamba atabaki kuwa mmiliki wa eno hilo na endapo huyo mvamizi ataendelea kumsumbua awasiliane na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete.

Kampeni hiyo ilikuwa inafanyika katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Njombe baada ya kuzinduliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Doto Biteko Mei 26, 2024 imekamilika leo Juni 4, 2024.