Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wananchi Wajitokeza Kupata Elimu ya Sheria Kwenye Maonesho ya Nanenane

Imewekwa: 07 Aug, 2023
Wananchi Wajitokeza Kupata Elimu ya Sheria Kwenye Maonesho ya Nanenane

Na. George Mwakyembe - WKS Mbeya. 

Banda la Wizara ya Katiba na Sheria lililopo katika viwanja vya maonesho ya Nanenane katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya ambapo maonesho haya kwa mwaka huu yanafanyika Kitaifa na Kimataifa mkoani humo limeendelea kupokea wateja kwa wingi wanaofika kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria.

Miongoni mwa wateja wanaotembelea banda hilo ni wanafunzi ambao walitaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu elimu ya ukatili wa kijinsia na nini wanachotakiwa kufanya mara mtu wanapopatwa na janga hilo. Pia watu mbalimbali wamekuwa wakifika kwa wingi kupata elimu ya sheria pamoja na msaada wa kisheria. Kundi kubwa la wananchi wamekuwa wakiuliza maswali yanayohusu uandikaji wa wosia, haki za binadamu pamoja na kupata msaada wa kisheria wa namna ya kutatua migogoro ya ardhi, mirathi pamoja na ndoa.  

Maonesho ya Nanenane yanafanyika kwa mara ya kwanza Kimataifa jijini hapa lakini ikiwa ni ya tisa kufanyika mkoani Mbeya Kitaifa yakiongozwa na kauli mbiu “Vijana na Wanawake ni Msingi imara wa mifumo ya Chakula”. Maonesho haya yatafikia tamati Agosti 8 huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.