Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wananchi waomba vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri zaidi ya miaka mitano vitolewe kwenye Ofisi za Kata

Imewekwa: 27 Jul, 2023
Wananchi waomba vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri zaidi ya miaka mitano vitolewe kwenye Ofisi za Kata

Na William Mabusi – WKS Tunduru

Wananchi wa vijiji vya Chiwana, Umoja na Mkandu wilayani Tunduru wameiomba Serikali kuweka utaratibu ili vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri zaidi ya miaka mitano navyo vitolewe kwenye Ofisi za Kata kama ilivyo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili kuwapunguzia gharama na muda wa kufuatilia vyeti hivyo kwenye ofisi za Wilaya ambazo kwa baadhi ya Kata ofisi hizo ziko mbali.

Ombi hilo limetolewa kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara iliyoitishwa na timu inayotekeleza kampeni ya msaada wa sheria ya Mama Samia Wilayani humo, tarehe 26 Julai, 2023.

“Tunaipongeza Serikali kwa kusimamia utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano kwenye ofisi za Kata. Tunaiomba Serikali kuweka utaratibu ili watoto wenye umri zaidi ya miaka mitano nao waweze kupata vyeti vyao kwenye ofisi zetu za Kata.” Alisema mzee Mapepe Said kutoka Kijiji cha Chiwana.

Akitoa elimu ya usajili wa vizazi na vifo kwenye mikutano hiyo Bw. Mwinyijuma Maneno Moshi Afisa Msajili Msaidizi kutoka RITA ambaye yuko kwenye timu ya wataalam wanaotekeleza Kampeni hiyo amesema watoto walio na umri chini ya miaka mitano husajiliwa bure bila malipo na kupewa vyeti vya kuzaliwa ndani ya siku tisini tokea mama alipojifungua.

Timu ya wataalam wanaotekeleza Kampeni hiyo Wilayani Tunduru imeshafikia Kata nane kati ya ishirini zinazotakiwa kutekelezwa katika kipindi cha siku kumi tangu kuzinduliwa kwa Kampeni hiyo mkoani Ruvuma. Kata ambazo zimefikiwa hadi sasa ni Muungano, Nanjoka, Nakapanya, Nandembo, Lukumbule, Mchoteka, Marumba na Chiwana.

Kampeni hiyo ilizinduliwa na Mhe. Dkt. Philip Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Julai, 2023 mjini Songea na mara baada ya uzinduzi wataalam waligawanyika kutekeleza kampeni hiyo kwenye Halmashauri zote nane katika Mkoa wa Ruvuma.