Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wananchi wapongeza Mama Samia Legal Aid Campaign

Imewekwa: 06 May, 2023
Wananchi wapongeza Mama Samia Legal Aid Campaign

Na William Mabusi - WKS Dodoma

Wananchi waliofikiwa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia wamepongeza jitihadi za uongozi wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na mkakati wa kuwafikia wananchi wengi wa hali ya chini katika kuwapatia elimu ya sheria kupitia Kampeni hiyo ambayo kwa sasa inaendelea kwenye Halmashauri zote za Jiji la Dodoma.

Mmoja wa wananchi hao ni Diwani wa Kata ya Mtumba Mhe. Edward Maboje ambaye ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria kuiangalia Kata ya Mtumba kwa jicho la kipekee kwani Mtumba ndiyo kata mama na kitovu cha Serikali.

“Hii ni nafasi ya pekee ambayo Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaitumia kuwafikia wananchi wa chini kutatua kero zao za kisheria na upatikanaji haki.” Alisema Mhe. Maboje wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara kwenye kata yake Tarehe 04 Mei, 2023. 

Kwa upande wake Elizabeth Kinyalwa, Mkazi wa kijiji cha Vihingo wilayani Kongwa amesema elimu hii imekuwa msaada mkubwa hasa kwa upande wa wanawake kwenye upande wa mirathi kwani wanawake wamekuwa wakidhulumiwa mali na ndugu wa mwanaume pindi umauti unapomkuta mume na wao hawakujua wapi pa kuanzia katika kudai haki zao.

“Ni kawaida hapa kwetu mara mume anapofariki mwanamke hunyang’anywa mali zote ambazo kashirikiana na mumewe kuzichuma na watoto pia wanachukuliwa huku mwanamke akiachwa bila kitu kwa kigezo kuwa ataolewa tena, hivyo tunamshukuru sana Rais wetu na Wizara yenu kutuletea elimu hii.” Alisema bibi Elizabeth.

Kampeni hii ilizinduliwa Jijini Dodoma Aprili 27, 2023 na Mhe. Kassim Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanza kutekelezwa rasmi Jijini Dodoma kwa siku kumi kuanzia tarehe 28 Aprili, 2023 ambapo Halmashauri zote nane yaani Dodoma Jiji, Chamwino, Mpwapwa, Kongwa, Chemba, Bahi, Kondoa DC na Kondoa TC katika Jiji la Dodoma zitafikiwa.

Mama Samia Legal Aid Campaign ni kampeni inayotekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Rais-Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali na wasio wa Serikali imelenga kuimarisha mfumo wa utoaji haki ambapo kupitia kampeni hiyo wananchi wengi nchini watapewa elimu ya sheria na wenye mgogoro mbalimbali inayohusu ardhi, unyanyasaji wa kijinsia, ndoa, mirathi watapewa huduma ya msaada wa kisheria.