WASULUHISHI WAONGEZEWA MBINU ZA UTATUZI WA MIGOGORO YA KAZI
Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) pamoja na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), imeanza mafunzo maalum kwa wasuluhishi na waamuzi kutoka mikoa mbalimbali nchini, yenye lengo la kuimarisha matumizi ya mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR) ili kuhakikisha mazingira salama na yenye tija mahali pa kazi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu, Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Utatuzi wa Migogoro kwa njia mbadala wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Felix Chakila, amesema kuwa migogoro mingi ya kikazi husababishwa na maslahi binafsi, ukiukwaji wa mikataba, pamoja na mapungufu katika utekelezaji wa sheria na taratibu.
Ameeleza kuwa kuimarishwa kwa mbinu za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kutasaidia kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani, na hivyo kuchochea ufanisi katika shughuli za uzalishaji pamoja na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla, amesema kuwa mafunzo hayo yanahusisha washiriki kutoka mikoa yote pamoja na wilaya sita, yakilenga kuwaongezea ujuzi na uwezo wa kushughulikia migogoro ya kikazi kwa ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, washiriki watapata fursa ya kujifunza mbinu za kisasa za usuluhishi zitakazowawezesha kwenda sambamba na mabadiliko ya wakati na kuongeza tija katika utendaji wao.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Annamarie Kiaga, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kikazi yenye staha kati ya waajiri na wafanyakazi, hali itakayochangia ustawi wa sekta ya ajira nchini