Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Watendaji wa Serikali Wajengewa Uwezo Juu ya Mikataba ya Haki za Binadamu

Imewekwa: 29 Nov, 2024
Watendaji wa Serikali Wajengewa Uwezo Juu ya Mikataba ya Haki za Binadamu

Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Jumuiya ya Madola na Ofisi ya Balozi Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Kanda ya Afrika Mashariki imeandaa mafunzo kwa Maafisa wa Serikali juu ya uwasilishaji wa ripoti za utekelezaji wa Mikataba ya Haki za Binadamu ambayo Serikali imeridhia ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu.

Akizungumza leo tarehe 28 Novemba, 2024 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu  yanayofanyika katika Hoteli ya Morena mjini Morogoro, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili Salimu Msemo akimwakilisha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini amesema kuwa  ni vyema Wataalamu hao kutumia mafunzo hayo ili kuongeza ujuzi katika kuandaa na kutoa taarifa muhimu juu ya Mikataba ya Haki za Binadamu na Wajibu wa Serikali nchini ya kila kifungu.

"Kama watumishi wa Umma, nawakumbusha kuwa wasikivu ili lengo la Serikali la kuongeza  uwezo wenu katika kutekeleza majukumu yenu litimie.Tunahitaji muwasilishe taarifa ili kuweza kukamilisha ripoti ya juhudi za Serikali za kukuza na kulinda haki za watu wenye ulemavu."Alisema Salimu

Sambamba na hilo Salimu   amesema kuwa  katika utekelezaji wa Mikataba  Serikali inatakiwa kutoa taarifa ya namna ilivyotekeleza Mikataba hiyo kwa kuchukua hatua za Kisera,Kikanuni, Kitaasisi na Kiutawala.

Kwa upande wake Mshauri wa Haki za Binadamu kutoka Ofisi ndogo za Umoja huo zilizopo Geneva, Yashasvi Nain amesema Tanzania inatekeleza mikataba sita kati ya tisa ya msingi ya Kimataifa ya Haki za Binadamu hivyo Serikali ina wajibu wa kufuatilia na kutoa taarifa za mara kwa mara kwa vyombo husika vya mkataba kuhusu jinsi ahadi hizi za kimataifa zinavyotafsiriwa katika hatua na utekelezaji wa kitaifa na inahitaji rasilimali kubwa, pamoja na uwezo wa kibinadamu na kiufundi. 

Rai imetolewa kwa Wizara na Taasisi zinazohusika kuendelea kutoa ushirikiano ili kuipatia Wizara ya Katiba na Sheria mifano ya Sera, Sheria, Programu na takwimu zilizogawanywa kutoka Ofisi zinazohusika ili kuepuka kuwa na ripoti zenye ubora duni.