Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Watumishi wa Wizara wahimizwa kudumisha umoja

Imewekwa: 24 Mar, 2023
Watumishi wa Wizara wahimizwa kudumisha umoja

William Mabusi na Farida Khalfan - WKS 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewahimiza Watumishi na Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria kudumisha umoja na kufanya kazi kwa kuaminiana katika kutekeleza majukumu ya Wizara.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo tarehe 24 Machi, 2023 Jijini Dodoma.

“Katika eneo la kazi hakuna kitu muhimu kama umoja, mkikosa umoja hamwezi kufanikisha kazi zenu.” Alisema Dkt. Ndumbaro.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema umoja na ushirikiano katika utendaji kazi utawezesha Wizara kutekeleza majukumu yake katika mwaka ujao wa fedha huku akiyataja baadhi ya majukumu hayo ambayo ni Usimamizi wa mchakato wa Katiba mpya; Ushiriki wa nchi katika mikutano ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa inayoshughulika na masuala ya haki za binadamu; Ushiriki wa Wizara katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia; Kufanya marekebisho ya Sheria zinazohusiana na Demokrasia, Vyama Vingi vya Siasa na Uchaguzi na Kanuni zake.

Pia Dkt. Ndumbaro amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuunda Tume ya Haki Jinai ambapo mlaji wa taarifa zinazotolewa na Tume hiyo ni Wizara ya Katiba na Sheria katika kusaidia kuboresha maeneo mbalimbali yanayohusu mfumo wa haki jinai.

Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amewataka Watumishi na Menejimenti ya Wizara kuongeza ubunifu wa mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto kwenye sehemu zao za kazi ili kuongeza ufanisi na tija katika kuwahudumia watazania.

Vikao vya Baraza la Wafanyakazi ni moja ya fursa ya kufanya mawasiliano kati ya menejimenti na wafanyakazi ambapo Wafanyakazi hupokea mipango ya Menejimenti na Menejimenti hupokea mapendekezo kutoka kwa wafanyakazi.