Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Watumishi watakiwa kutumia lugha nzuri maofisini

Imewekwa: 23 Jul, 2023
Watumishi watakiwa kutumia lugha nzuri maofisini

Na William Mabusi - WKS Tunduru

Wakazi wa vijiji vya Majengo, Muungano na Kalanje wamewataka watumishi wa umma kutumia lugha nzuri kwa wananchi hasa pale wanapofika kwa ajili ya kupata huduma katika ofisi zao.

Rai hiyo imetolewa na wananchi hao wakati wa utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign wilayani Tunduru ambapo timu ya wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Wadau washirika walipofika katika vijiji hivyo kwa lengo la kutoa elimu na msaada wa kisheria leo 23/07/2023.

Kwa pamoja wananchi hao walionekana kufurahishwa na elimu iliyotolewa na kusema ilikuwa ni bahati  kubwa kwao kupata elimu ya sheria na migogoro yao kutatuliwa lakini hali huwa haiwi hivi wakifika maofisini.

Wanachi hao wakatumia kampeni hiyo kuwaomba watumishi wa umma kutumia lugha nzuri na maneno mazuri kama ambayo wameyatumia wakati wa kutoa elimu hiyo.

“Mmetumia maneno mazuri wakati wa kutoa elimu, tunawaomba tunapokuja ofisi zenu mtusikilize na kutujibu kwa sauti na lugha nzuri kama mlivyofanya leo,” alisema Bi. Lucy Jacob Chibwanga.

Aidha, Bi. Chibwanga aliongeza kuwa “maana unaenda ofisini kutoa shida yako unapewa taarifa nusu ama iliyopotoshwa au basi tu hupewi ushirikiano halafu unaenda kufanya jambo kumbe umefanya kinyume na taratibu, mfano kama jambo hilo lilikuwa ni ujenzi unakuja kuvunjiwa kibanda.”

Akitoa mada ya ardhi kwenye mkutano huo Bw. Kyema Paul Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Tunduru amewataka wananchi kuepuka uuzaji holela wa mashamba kwa wafugaji. “Mashamba ni maeneo yaliyotengwa kwa kilimo, mfugaji akishamiliki eneo hilo huingiza mifugo yake kulisha kitu ambacho hupelekea migogoro kati ya wafugaji na wakulima.”

Uzinduzi wa utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign katika Mkoa wa Ruvuma umefanyika Julai 22, 2023 kwenye viwanja vya Majimaji mjini Songea ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Philip Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wataalam wanaotekeleza kampeni hiyo mkoani humo wamesambaa kwenye Halmashauri zote nane ambapo zoezi hilo litafanyika kwa siku kumi.