Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Waziri Chana Awasilisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria Kwenye Kamati ya Bunge

Imewekwa: 19 Oct, 2023
Waziri Chana Awasilisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria Kwenye Kamati ya Bunge

Na George Mwakyembe & William Mabusi - WKS Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewasilisha Mswada wa marekebisho ya sheria 23 kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yaliyolenga kuondoa upungufu uliobainika wakati wa utekelezaji wa sheria hizo.

Mhe. Chana amewasilisha mapendekezo ya marekebisho hayo tarehe 18 Oktoba, 2023 kwenye ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.

Mhe. Chana amezitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora sura ya 391 (The Commission for Human Right and Good Governance Act, Cap 391) na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki Sura ya 442 (The Electronic Transaction Act, Cap 442) miongoni mwa zingine ili kuendana na wakati.

Akichangia kwenye kikao hicho mjumbe wa Kamati ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Rashid Abdallah Shangazi ameeleza kuwa marekebisho ya sheria hizo lazima yazingatie wakati pamoja na tafiti ili ziendane na wakati. Akifafanua zaidi kwenye Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai sura ya 20 (The Criminal Procedure Act, Cap 20) amesema “Mashauri mengi yamekuwa yakicheleweshwa mahakamani hata kama ushahidi upo lakini bado mtuhumiwa anachukua muda mrefu pasipo na hukumu.” Kuhusu wahamiaji haramu alishauri Serikali kuwa na sheria ya kuwarudisha makwao kuliko kuwakamata na kuwajaza kwenye Magereza yetu.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Florent Kyombo ameshukuru Wizara kwa marekebisho hayo ambayo yataleta mabadiliko ya kutekeleza sheria hizo katika jamii zetu. “Nawashukuru sana Wizara na watalaam kutoka Taasisi zake kwa kuleta mapendekezo haya ya marekebisho ya sheria, imani yangu yataleta mafanikio kwenye jamii zetu,” alisema Mhe. Kyombo.

Baada ya wajumbe wa Kamati kumaliza kutoa maoni na mapendekezo yao, Mhe. Chana aliwashukuru wajumbe wote kwa michango yao na ushirikiano wanaotoa kwa Wizara na kuahidi kuyafanyia kazi  mapendekezo yote ambayo wameyatoa.