Waziri Chana na Balozi Possi Wakubaliana Kuimarisha Utendaji Kazi wa Watumishi

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Geneva, Switzerland
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Geneva Switzerland Mhe. Balozi Dkt. Abdallah Possi ambapo Waziri Chana alitumia nafasi hiyo kumwomba Balozi Possi kuangalia fursa mbalimbali ambazo watumishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wanaweza kuzipata hapa Geneva.
Waziri Chana amezungumza hayo leo tarehe 01/07/2024 alipofika katika katika Ofisi ya Ubalozi jijini Geneva ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Mhe. Waziri na ujumbe wake katika kikao cha 56 cha Baraza la Haki za Binadamu kinachoendelea jijini Geneva - Switzerland.
Akizitaja fursa hizo, Waziri Pindi Chana alisema ushiriki wa wataalam wetu katika vikao na warsha mbalimbali ni muhimu lengo likiwa ni kuhakikisha nchi inapata uwakilishi wa kutosha katika maeneo mbalimbali na hivyo kutangaza vizuri nchi yetu katika anga za kimataifa lakini pia watumishi wakiongeza uelewa katika utendaji kwa kubadilishana uzoefu na watumishi kutoka mataifa mengine.
Aidha, Waziri Pindi Chana akaongeza kuwa kutokana na maendeleo ya kiteknolojia Balozi anaweza watafutia nafasi za kushiriki warsha kwa njia ya mtandao (Zoom n.k) ambavyo si lazima mshiriki kuwepo eneo ambalo mkutano unafanyikia.
Akizungumza baada ya maelezo ya Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema Wizara kwa upande wa Tanzania Bara kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaendelea kuimarishwa nchini Tanzania. Aidha, akasisitiza kwa upande Ubalozi kuweza kutafuta nafasi mbalimbali zikiwemo internship kwa lengo la kuongeza uwezo wa kufikiri kwa wataalam baada ya kupata uzoefu kutoka mataifa mengine.
Akiongelea kuhusu suala la kujengea uwezo watumishi, Balozi Possi alikubali kuwa suala hilo ni mtambuka na lina tija hivyo akaomba yaainishwe mahitaji kwa maandishi katika maeneo ambayo Wizara ingependa wataalam wajengewe uwezo ili yeye na Ofisi yake aweze kuwasiliana na Wadau na kuona jinsi ya kuliwezesha hilo huku akikiri kuwa suala hilo linatekelezeka.
Kikao cha 56 cha Baraza la Haki za Binadamu kinaendelea leo jijini Geneva- Switzerland katika ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo leo mada iliyojadiliwa ni kuhusu utunzaji wa mazingira na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.