Waziri Kabudi Apokea Taarifa Nane za Mapitio ya Sheria

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea taarifa nane za tafiti za mapitio ya Sheria zilizofanywa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 na Tume ya Kurekebisha Sheria Nchini (LRCT), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Tume katika kufanya tafiti na mapitio ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuziboresha na kuzifanya ziendane na wakati uliopo.
Akiwasilisha taarifa ya tafiti hizo wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika Oktoba 16, 2024 katika ukumbi wa Wizara Mtumba, jijini Dodoma Mwenyekiti wa Tume ya Kurebisha Sheria Mhe. Jaji Winfrida Korosso amesema kuwa maandalizi ya taarifa hizo yamehusisha hatua mbalimbali ikiwemo uchambuzi wa hoja za awali, tafiti, mapitio ya uwandani, ukusanyaji na uchambuzi wa maoni ya wadau na maandalizi ya taarifa husika.
Kwa upande wake Waziri Kabudi ameipongeza Tume kwa kazi inayofanya katika kufanya maboresho ya Sheria yenye tija na amesema kuwa taarifa hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai katika kusimamia mnyororo mzima wa utoaji Haki Nchini ili kuimarisha Utawala Bora na kulinda Utu wa Binadamu.
"Tunahitaji kufanya mageuzi ya kimuundo na kuifanya Tume kuwa taasisi ya utafiti inayojitegemea ambayo itakuwa chanzo cha fikra za Kisheria cha Serikali (think tank) kama zilivyo taasisi nyingine za utafiti hapa Nchini."
Waziri Kabudi aliendelea kusema "Sekta ya Sheria inapitia changamoto na adha mbalimbali hususan za kiutendaji katika mchakato wa upatikanaji wa Haki kwa wakati ambapo Wizara pamoja na taasisi zake inaweka mifumo rahisi itakayowezesha Taasisi za usimamizi wa Sheria na utoaji Haki zinastahimili mahitaji ya jamii kwa mujibu wa Sheria za Nchi na kuimarisha utawala Bora."
Waziri Kabudi ametoa rai na amesema Wizara itaanda mapendekezo na kuona namna itakavyoweza kulifanya kuwa takwa la Kisheria kwa taasisi zote Nchini zinazohitaji kufanya Marekebisho ya Sheria kupeleka mapendekezo yao ya nia ya kufanya Marekebisho ya Sheria kwenye Tume ya Kurekebisha Sheria ili ifanye utafiti na kutoa mapendekezo ya maboresho ya Sheria ili kuhakikisha yanatija kwa Taifa.