Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WAZIRI MKUU APONGEZA WIZARA ZA KATIBA NA SHERIA BARA NA ZANZIBAR

Imewekwa: 16 Jun, 2025
WAZIRI MKUU APONGEZA WIZARA ZA KATIBA NA SHERIA BARA NA ZANZIBAR

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amezipongeza Wizara ya Katiba na Sheria Bara na Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar kwa kutekeleza kikamilifu na kwa ufanisi maono ya Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanapata haki zao.

Mhe. Majaliwa amebainisha hayo leo Juni 16, 2025, wakati akimuwakilisha Rais Samia kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia Jijini Dar Es Salaam,akieleza kuwa kampeni hiyo ni mahususi kwaajili ya kuondoa changamoto za kisheria kwa Watanzania.

"Niwapongeze Mawaziri wa Katiba na Sheria kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kule Zanzibar kwa kuendelea kusimamia kwa ufanisi mkubwa kabisa maono ya Kiongozi wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Watanzania wanatambua haki zao lakini pia kujua sheria zinazoweza kuwalinda na kulinda maslahi yao.", Mhe. Majaliwa.

 Ameongeza kuwa Kampeni hiyo ya msaada wa kisheria inatuma ujumbe maalum kwa watanzania kuwa wakati ni sasa wa Watanzania kujua haki zao huku akiwapongeza wananchi wa Dar Es Salaam kwa kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi wa Kampeni hiyo leo katika uwanja wa Maturubai Mbagala Jijini Dar Es salaam.