WAZIRI NDUMBARO AKUTANA NA BALOZI WA JAPAN KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA SHERIA

Dar es Salaam, Agosti 13, 2025
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Mikami Yoichi, Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili wamejadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika sekta ya Sheria, ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu katika uendelezaji sekta ya Sheria pamoja na kujengeana uwezo kati ya wataalamu wa Sheria kutoka pande zote mbili.
Mhe. Dkt. Ndumbaro amepongeza Serikali ya Japan kwa ushirikiano wake wa muda mrefu na Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mahusiano hayo hasa katika maeneo ya Utawala wa Sheria.
Kwa upande wake, Balozi Mikami Yoichi ameeleza utayari wa Serikali ya Japan kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kusaidia mageuzi ya sekta ya Sheria na kuhakikisha mfumo wa Haki unakuwa shirikishi, wa kisasa na unaozingatia misingi ya kimataifa.