Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Waziri Pindi Akutana na Balozi wa Singapore

Imewekwa: 22 Apr, 2024
Waziri Pindi Akutana na Balozi wa Singapore

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Mhe. Balozi Douglas Foo ambapo wameongelea na kukubaliana maeneo mbalimbali ya kufanya mafunzo na kubadilishana uzoefu.

Mazungumzo hayo yamefanyika Aprili 22, 2024 Ofisi za Bunge Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kutekeleza maazimio ya Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika mwezi Machi 2024 Zanzibar. Katika mkutano huo moja ya maazimio yaliyopitishwa ni nchi wanachama kubadilishana uzoefu katika sekta mbalimbali ikiwemo sheria, teknolojia na matumizi ya akili bandia.

Katika mazungumzo ya leo Mhe. Foo amesema Singapore iko tayari kutoa mafunzo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, suala ambalo limepokelewa kwa mikono miwili na Dkt. Chana. “Kama Wizara tunaona umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na tunaendelea kufungua Vituo vya Utatuzi wa Migogoro kwa mjia Mbadala nchini. Nimependezwa na ajenda hii muhimu ya mafunzo na imekuja kwa muda muafaka.”

Maeneno mengine ya kujifunza na kubadilishana uzoefu waliyokubaliana ni usalama wa taarifa za mtandaoni na mifumo ya TEHAMA, ushirikiano kwenye Taasisi za sheria kama Chama cha Wanasheria Tanganyika na Taasisi za Mafunzo ya Sheria.