WIZARA ITAHAKIKISHA BODI ZA USULUHISHI WA MIGOGORO YA NDOA ZINAFANYA KAZI KWA UFANISI

Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha bodi za usuluhishi wa migogoro ya ndoa zinafanya kazi kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia haki za binadamu hususan wanawake na watoto ambao mara nyingi huathirika zaidi katika migogoro ya ndoa.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kwa Umma Bi. Angela Anatory ameyasema hayo leo Septemba 30 2025 wakati akifunga rasmi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Eliakim Maswi, kikao cha kupitia na kuhakiki maudhui na mikakati ya kuimarisha Bodi za Usuluhishi wa Migogoro ya ndoa Tanzania Bara.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho Bi. Anatory amesema kuwa kikao hicho kimekuwa na mafanikio makubwa katika kujadili changamoto mbalimbali zinazozikumba Bodi hizo pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha utendaji kazi wake.
Kikao hicho kilijumuisha wawakilishi zaidi ya 50 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, Maafisa wa serikali, Wanasheria, Maafisa maendeleo ya jamii na kimefanyika kwa muda wa siku mbili Jijini Arusha.