Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA NA MAGEREZA KUSHIRIKIANA KUTOA MSAADA WA KISHERIA KWA WAFUNGWA NA MAHABUSU

Imewekwa: 11 Jun, 2025
WIZARA NA MAGEREZA KUSHIRIKIANA KUTOA MSAADA WA KISHERIA KWA WAFUNGWA NA MAHABUSU

Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupititia Jeshi la Magereza wameahidi kuendeleza ushirikiano katika kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu nchini.

Hayo yamebainishwa leo Mei 11,2025 na Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji Haki Wakili Jane Lyimo wakati wa mafunzo ya maafisa sheria na maafisa urekebu wa Jeshi la magereza ikiwa ni siku ya tatu tangu kuzinduliwa mafunzo hayo katika ukumbi wa Cate Convention Centre Morogoro.

 “Wizara na Magereza tuendelee kushirikiana katika kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu na ninatoa rai kwa maafisa sheria wa magereza muendelee kutoa msaada wa kisheria kwani huo ndio wajibu wetu kwa jamii pia kupitia mafunzo haya muendelee kutathmini ni maeneo yapi ambayo tunawerza kuimarisha ushirikiano katika kuwasaidia walioko mahabusu na magerezani”, amesisitiza Wakili Lyimo.

Naye Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Edith Shekidele ametoa mada kuhusu sheria ya Msaada wa Kisheria na Utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambapo amewaeleza maafisa hao kuwa kampeni hiyo imelenga kuwafikia wananchi walioko pembezoni na kupunguza malalamiko ya wananchi  wakati wa ziara za viongozi.

Amesema, “ Hadi sasa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imewafikia wananchi zaidi ya milioni mbili na laki saba, huku migogoro 25,299 ikiwasilishwa na migogoro 5853 ikitatuliwa, pia wafungwa na mahabusu 7570 walifikiwa na huduma hiyo, vituo vuy polisi 28 vimetembelewa na magereza 24 yamefikiwa na kampeni hiyo”, amefafanua Shekidele.

Ameongeza kuwa kupitia Kampeni hiyo wananchi wanapata elimu ya mirathi, wosia, haki za binadamu na utawala bora, ukatili wa kijinsia, utatuzi wa mogogoro kwa njia mbadala, uandaaji wa nyaraka za kisheria na uwakilishi katika vyombo vya utoaji haki ambapo huduma zote hizi hutolewa bure.