Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wizara Yaita Wadau Uboreshaji Wa Daftari la Orodha ya Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria

Imewekwa: 16 Jul, 2024
Wizara Yaita Wadau Uboreshaji Wa Daftari la Orodha ya Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria

Lusajo Mwakabuku – WyKS Dodoma.

Wizara ya Katiba na Sheria leo tarehe 16/07/2024 imeitisha kikao cha wadau kujadili uboreshaji wa Daftari la Orodha ya Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria linalotarajiwa kuzinduliwa rasmi mwishoni mwa mwezi wa nane, 2024.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Katiba na Sheria Mtumba Dodoma, kimejumuisha wataalam kutoka taasisi za Serikali na Asasi za Kiraia kimeazimia kuunda timu maalum ambayo itatengeneza daftari lenye taarifa bora zaidi na kuliwasilisha katika Menejiment ya Wizara kabla ya kuzinduliwa rasmi.

Lengo la daftari hili ni kusogeza zaidi huduma kwa wananchi ili pale mwananchi atakapohitaji huduma za Msaada wa Kisheria kutosafiri  umbali mrefu kufuata huduma hizo Wizarani na  badala yake kutumia daftari hilo kufahamu ni sehemu gani katika eneo alilopo kuna huduma na aina ya msaada anayoweza kupata.