WIZARA YAONGEZA UJUZI ULINZI NA USIMAMIZI WA RASILIMALI ASILIA ZA NCHI
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuimarisha usimamizi na ulinzi wa rasilimali za Taifa kwa kuwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo maalum yanayoendelea kufanyika.
Katika kufanikisha lengo hilo Wizara imewakutanisha na kuwapatia mafunzo kwa muda wa siku nne mjini Morogoro, maofisa viungo kutoka Wizara na Taasisi za kisekta zinazosimamia rasilimali za nchi ili kujengewa uwezo katika kusimamia na kulinda utajiri wa asili na maliasilia za nchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia, Bw. Everest Mashiba alieleza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuongeza weledi, uwajibikaji, uadilifu na ushirikiano miongoni mwa maofisa hao, ili kuboresha usimamizi wa maliasili na kuchangia kufikia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, alibainisha kuwa mafunzo hayo yanatoa fursa muhimu kwa washiriki kubadilishana uzoefu na kuimarisha uratibu wa taasisi mbalimbali. Serikali imeendelea kusisitiza matumizi bora ya rasilimali za Taifa kwa kuzingatia tija, uwazi na kuhakikisha manufaa yake yanawanufaisha wananchi wote.
Usimamizi wa Rasilimali za Nchi, Mifumo ya Kisera na Kisheria ya usimamizi wa hewa ukaa, na uhalisia wa utekelezaji wa dhana ya ushirikishwaji wa Wananchi katika miradi ya uwekezaji ni miongoni mwa mada ambazo zimejadiliwa katika kikao hicho.
Mafunzo haya yameandaliwa kwa lengo la kuimarisha weledi, ufanisi na ushirikiano miongoni mwa maofisa, ili kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumika kwa manufaa ya wote na kuunga mkono malengo ya maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika kufikia Dira ya Taifa 2050.