Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wizara yatoa Mafunzo ya Sheria kwa Waandishi wa Habari

Imewekwa: 10 Oct, 2023
Wizara yatoa Mafunzo ya Sheria kwa Waandishi wa Habari

Na William Mabusi – WKS Morogoro

Wizara ya Katiba na Sheria imeendesha Mafunzo kwa Waandishi wa Habari Waandamizi kutoka Vyombo mbalimbali vya Habari kuhusu Sheria na Kanuni za Ulinzi kwa Watoa Taarifa na Mashahidi zenye lengo la kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu kwa kuwatambua na kuwalinda watoa taarifa na mashahidi.

Mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku mbili yameanza tarehe 10 Oktoba, 2023 mkoani Morogoro yamefunguliwa na Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro, Bi. Neema Haule.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Bi. Neema Haule amesema Sheria na Kanuni hizo zitasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wale wote wanaotoa taarifa za uhalifu wa makosa ya aina mbalimbali wanayoshuhudia yakitendeka katika jamii inayowazunguka.

“Kanuni hizi zitakuwa msaada sana kwani pamoja na masuala ya ulinzi, lakini zinaweka taratibu za kuwalipa au kuwapa fidia watoa taarifa na mashahidi kutokana na madhara yatakayowapata ama kwa kutoa taarifa au kuhusika katika kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu.” Ameeleza Bi. Haule.

mafunzo haya yanatolewa kwa Wanahabari Waandamizi ili wawe mabalozi na kuuhabarisha umma kuhusu taratibu za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi kuwahamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kutoa taarifa kuhusu uhalifu unaotokea au unaotarajiwa kutokea katika jamii ambayo inatakiwa iwe sehemu salama kwa mwananchi kuishi kwa amani na utulivu.

“Niwaombe kupitia taaluma yenu ya habari tuendelee kutoa elimu ya kisheria kwa umma wa Watanzania kuhusiana na sheria na kanuni hizi ili wawe na uelewa na wajue umuhimu wa kuwafichua wahalifu wa makosa mbalimbali yanayotendeka katika jamii yetu ili mwisho wa siku matukio ya kiuhalifu yaweze kupungua na kuisha kabisa.” Alisema.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Burton Mwasomola amesema lengo la Sheria na Kanuni hizo ni kufichua maovu katika jamii, makosa ya kiuhalifu ikiwemo ukiukwaji wa maadili kwa watumishi wa umma.

Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi, Ufuatiliaji na Tathmini Programu ya Building Sustainable Ant Corruption Action in Tanzania (BSAAT), Ofisi ya Rais, Ikulu, Bw. Josiah Mathania amesema kadri elimu hiyo inavyozidi kutolewa, wananchi wataweza kutoa taarifa bila uoga kama ilivyokuwa awali.

“Programu inaamini kuwa baada ya mafunzo haya, wananchi watapata uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni hizi kupitia Vyombo vyenu vya Habari, na hivyo kupelekea kufanikisha kiashiria kikuu cha kwanza cha program ya BSAAT cha kuongeza taarifa shuku za rushwa/uhalifu,” amesema na kutaja viashiria vingine viwili vya BSAAT kuwa ni kupunguza muda wa kesi mahakamani na kurejesha/kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa.

Akielezea kuhusu Programu ya BSAAT, amesema ni Programu ya kujenga mfumo endelevu wa kupambana na rushwa nchini ambapo lengo kuu ni kuisaidia Serikali ya Tanzania katika juhudi zake za kupambana na rushwa kwa kuziwezesha Taasisi kumi ambazo moja ya majukumu yake ni kupambana na rushwa nchini.

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Wizara ya Katiba na Sheria, TAKUKURU, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Ofisi ya Msajili wa Makampuni, Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu, Mahakama ya Tanzania, Idara ya Utawala Bora na Maboresho, Ikulu.

Akichangia katika mafunzo hayo mwandishi kutoka Fullshangweblog.co.tz Bw. John Bukuku amependekeza kuwepo na udhibiti wa taarifa inayotolewa kwenye vyombo vya uchunguzi ili mamlaka hizo zisiwe na mwanya wa kupindisha taarifa ya kweli kuifanya ya uongo na hivyo mtoa taarifa kujikuta anapewa kesi kwamba ametoa taarifa ya uongo.