Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA  YAWANOA  MAWAKILI NA MAAFISA SHERIA KUHUSU  UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA MBADALA

Imewekwa: 17 Mar, 2026
WIZARA  YAWANOA  MAWAKILI NA MAAFISA SHERIA KUHUSU  UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA MBADALA

Wizara ya Katiba na  Sheria imetoa  mafunzo kwa Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kutoka Sekretarieti  za Mikoa kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu mbinu za utatuzi wa migogoro  kwa njia mbadala(ADR), ili kuongeza ufanisi katika kushughulikia upatikanaji wa haki kwa wakati na kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani kwa kushughulikia migogoro nje ya Mahakama. 

Akifungua rasmi mafunzo  ya Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali  tarehe 16 Machi, 2026 Kibaha mkoani Pwani, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Pwani Dkt. Kusirye Ukio akimuwakilisha Katibu Tawala mkoa wa Pwani Bi. Pili Mnyema amesema ni muhimu sasa Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kuongeza nguvu katika kutatua migogoro ya wananchi kwa njia mbadala ili kurahisisha upatikanaji  wa  haki kwa wananchi, kuondoa uhasama na kujenga mahusiano mazuri katika jamii. 

"Ni muhimu watalaam hawa wakisheria kuendelea kujifunza na kujengewa uwezo kuweza kukabiliana na changamoto kwa weledi na kwa ufanisi katika kuhudumia watanzania" amesema Ukio. 

Aidha, Ukio amesisitiza kuwa ulimwengu sasa umejikita katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii kwa njia Mbadala kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu kitu ambacho kimewanufaisha watanzania walio wengi wasioweza kukidhi gharama za huduma.