ZAIDI YA WANANCHI MILIONI 4 WAMEFIKIWA NA MSAADA WA KISHERIA

Wizara ya Katiba na Sheria imebainisha kuwa zaidi ya wananchi milioni 4 wamefikiwa na huduma za msaada wa kisheria katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambapo Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imetekelezwa katika mikoa yote 31, ikiwemo 26 ya Tanzania Bara na 5 ya Tanzania Visiwani.
Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi, ametoa taarifa hiyo leo, Agosti 12, 2025 jijini Dodoma, wakati akichangia mada katika Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) linalofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Bi. Msambazi, ambaye pia ni Msajili wa Mashirika ya Msaada wa Kisheria nchini, amesema kuwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa Kushirikiana na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yaliyosajiliwa wamewezesha kusajili migogoro zaidi ya 26,000, pamoja na kutatua migogoro zaidi ya 6,000 ya papo kwa papo ambayo imepatiwa ufumbuzi mara moja.
Aliongeza kuwa kasi ya utiaji Huduma za Msaada wa Kisheria hada katika maeneo ya vijijini imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano baina ya Wizara na Nashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Mikakati mingi ya utoaji haki inayotekelezwa na serikali ya awamu ya Sita.
“Tunayapongeza mashirika haya kwa mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, lakini pia tunasisitiza umuhimu wa kuwa na vyanzo vya ndani vya rasilimali fedha ili kuepuka utegemezi kwa wadau wa maendeleo,” alisema Bi. Msambazi.
Katika kongamano hilo, wadau walihimizwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na serikali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata haki zao kwa wakati.