SERIKALI YACHUKUA HATUA MADHUBUTI KUHAHAKISHA HAKI ZA WANAWAKE NA WASICHANA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imewasilisha juhudi mbalimbali zinazolenga kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana, katika Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea katika Jiji la New York, nchini Marekani.
Akizungumza katika mkutano wa pembezoni uliofanyika machi 16, 2026 jijini humo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Uratibu wa Msaada wa Kisheria, Bi. Lucy Diganyeck ameeleza kuwa serikali imechukua hatua madhubuti katika kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki zao kwa urahisi.
Alitaja baadhi ya jitihada hizo kuwa ni pamoja na utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambapo kupitia kampeni hiyo Takriban wanawake 2,135,902 walifikiwa na walipatiwa huduma za msaada wa kisheria.
Katika hatua nyingine Diganyeck ameeleza jitihada za matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za kisheria kwa wanawake ambapo kupitia kituo cha huduma kwa mteja cha Wizara kimewezesha kutoa msaada wa haraka kupitia simu, hususan kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yenye changamoto za kijiografia na miundombinu.
Mkutano huo unaendelea ukiwa na kaulimbiu isemayo: “Kuimarisha Upatikanaji wa Haki kwa Wanawake na Wasichana Wote: Mchango wa Huduma za Msaada wa Kisheria katika Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia na Kufikia Uwezeshaji wa Wanawake Wote.”