Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

CHANGAMOTO ZA KISHERIA KUTATULIWA KIDIJITALI

Imewekwa: 17 Mar, 2026
CHANGAMOTO ZA KISHERIA KUTATULIWA KIDIJITALI

Wizara ya Katiba na Sheria imezindua rasmi huduma ya “Sema na Waziri” kupitia kituo chake cha huduma kwa mteja leo Machi 17, 2026, Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, amesema kuwa huduma hiyo imeanzishwa kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanafikiwa kwa njia mbalimbali na kupatiwa huduma kwa urahisi zaidi.

“Hii programu ya ‘Sema na Waziri’ ni muendelezo wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba lazima tusikilize changamoto za wananchi ili waweze kupata unafuu, hususan katika masuala ya kisheria. Wananchi wanaweza kuwasiliana nasi kupitia namba 0262160360 au 0800004004, pamoja na WhatsApp namba 0739101910,” amesema Mhe. Homera.

Aidha, ameongeza kuwa programu hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, na itakuwa ikifanyika angalau mara tatu kwa mwezi, ambapo Waziri atakuwa akizungumza moja kwa moja na wananchi kupitia kituo hicho.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, amesema kuwa wananchi wataendelea kupatiwa huduma stahiki na kubainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, jumla ya malalamiko 2,023 yamepokelewa, yakihusisha masuala ya ardhi, ndoa, mirathi, matunzo ya watoto, talaka, ukatili wa kijinsia, pamoja na kazi na ajira ambapo kati ya malalamiko hayo, jumla ya 1,394 tayari yamefanyiwa kazi.