Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

DKT.SHEKALAGHE AAHIDI ZAWADI NONO TIMU YA KATIBA SPORTS CLUB MASHINDANO YA SHIMIWI

Imewekwa: 19 Sep, 2026
DKT.SHEKALAGHE AAHIDI ZAWADI NONO TIMU YA KATIBA SPORTS CLUB MASHINDANO YA SHIMIWI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe, ameahidi kutoa zawadi nono kwa wachezaji wa timu ya Katiba Sports club iwapo watashinda mchezo wowote watakaoshiriki kwenye Mashindano ya Michezo ya Idara na Taasisi za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu.Dkt.Shekalaghe ametoa ahadi hiyo leo, Septemba 18, 2026, jijini Dodoma wakati akikabidhi vifaa vya michezo kwa wachezaji hao wanaojiandaa kuelekea kwenye mashindano hayo ya kitaifa.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dkt.Shekalaghe amewataka wachezaji hao kuhakikisha wanakwenda kushindana kwa nidhamu huku wakizingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.

“Nendeni mkashindane na sio kushiriki, mkiwa na morali kama timu ya Simba na ujasiri kama timu ya Yanga, mkiunganisha hayo mawili hakika mtarudi na ushindi; pia mzingatie miongozo na maadili ya utumishi wa umma ili kujenga mahusiano bora na washiriki kutoka taasisi zingine,” alisema Dkt.Shekalage.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara, Bw. Alfred Dede, ameeleza kuwa Wizara imeweka mazingira yote sawa ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa kwenye hali nzuri ya ushindani na inapeleka jumla ya washiriki 48, ambapo Miongoni mwao, washiriki 20 wanatoka kwenye taasisi zilizo chini ya Wizara, zikiwemo Taasisi ya Mafunzo ya Ujaji (IJA), Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA), na Shule ya Sheria Tanzania (LST).

Awali, akimkaribisha Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utawala, Bw. Peter Bunyazu, alisema Wizara inaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za kuhamasisha watumishi wa umma kujenga afya zao kupitia michezo, ndio maana imewawezesha watumishi hao kikamilifu ili wakalete ushindi.

Naye Kiongozi wa Msafara huo, Wakili Binto Mwangwa, amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa timu hiyo iko tayari na ina morali kubwa ya ushindi na kuwa watashiriki kwenye michezo sita  ambayo ni mpira wa miguu, mpira wa pete (netiboli), bao, riadha, kuvuta kamba na mchezo wa shabaha (datsi).

Mashindano ya SHIMIWI ya Kitaifa kwa mwaka 2026 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 20 Septemba 2026 mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Moshi, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, na yatahitimishwa tarehe 7 Oktoba 2026.