Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ELIMU YA SHERIA YAENDELEA KUTIKISA VYUO VIKUU

Imewekwa: 30 Apr, 2026
ELIMU YA SHERIA YAENDELEA KUTIKISA VYUO VIKUU

Wizara ya Katiba na Sheria kupitia kampeni ya msaada wa Kisheria wa Mama Samia (MSLAC) imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya kisheria kwa makundi mbalimbali ya jamii, huku ikiwafikia wanafunzi wa Vyuo vikuu kwa lengo la kuwajengea uelewa wa matumizi sahihi ya teknolojia katika kusaidia upatikanaji wa haki Nchini.

Akizungumza na wanafunzi Pamoja na watumishi katika mdahalo ulifanyika chuo Kikuu cha Mipango Jijini Dodoma tarehe 29 Aprili, 2026 Dkt.  Kulwa Gamba, mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alisema kuwa maendeleo ya teknolojia yamefungua milango mipya ya utoaji wa huduma za kisheria, na hivyo kuwapa wananchi nafasi ya kupata msaada wa kisheria kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

“Matumizi ya mifumo ya kidigitali kama majukwaa ya mtandaoni, programu za simu na mitandao ya kijamii yamekuwa nyenzo muhimu katika kutoa elimu ya sheria, kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki na hata kupata ushauri wa kisheria kwa wakati” alisema Gamba.

Dkt. Gamba alisisitiza kuwa pamoja na faida hizo, ni muhimu kwa watumiaji wa teknolojia kuwa waangalifu ili kuepuka kuvunja sheria, hasa katika matumizi ya mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakijihusisha na vitendo vinavyoweza kusababisha madhara ya kisheria bila kujua.

Aidha, alibainisha kuwa teknolojia inaweza kuwa chombo madhubuti katika kuzuia ukatili wa kijinsia na aina nyingine za ukatili, kwa kuwezesha utoaji wa taarifa kwa haraka, kuhifadhi ushahidi wa kidigitali, na kusaidia wahanga kupata msaada kutoka kwa mamlaka husika.

Kwa upande wao, wanafunzi walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewapa mwanga mpya kuhusu namna wanavyoweza kutumia teknolojia si tu katika taaluma zao, bali pia katika kulinda haki zao na za wengine katika jamii.

Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kusisitiza kuwa elimu ya kisheria ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, kwani inawajengea wananchi uwezo wa kutambua haki zao na wajibu wao, na hivyo kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za serikali za kuhakikisha kuwa wananchi, hususan vijana wa vyuo vikuu, wanakuwa mabalozi wa haki na sheria kwa kutumia teknolojia kwa njia sahihi, salama na yenye manufaa kwa jamii nzima.