Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

SERIKALI KUYAFANYIA UCHAMBUZI WA KISHERIA MABARAZA YA ARDHI

Imewekwa: 25 Sep, 2026
SERIKALI KUYAFANYIA UCHAMBUZI WA KISHERIA MABARAZA YA ARDHI

Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria  inaendelea na mkakati wa kufanya uchambuzi wa kina wa Sheria  inayosimamia Mabaraza ya Ardhi nchini ili kubaini kama mabaraza hayo yanahitaji kuongezewa nguvu na mamlaka ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha programu ya Sema na Waziri inayotekelezwa kupitia Kituo cha Huduma Kwa Mteja cha Wizara, Waziri wa  Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi  Homera amesema kuwa asilimia kubwa ya malalamiko yanayowasilishwa katika kipindi cha Sema na Waziri yanahusu migogoro ya ardhi jambo linalosababisha Serikali ijikite katika kuona namna ya kuyaongezea nguvu mabaraza hayo ama kuyahamishia majukumu hayo kwenye mahakama.

‘’Serikali  imedhamiria  kuichambua vizuri  Sheria  ya  Mabaraza ya Ardhi  ili kuweza kuyaongezea nguvu au kuweka mpango  wa  kuyahamisha  katika  Mahakama alisema Dkt. Homera.

Dkt. Homera amesema kuwa migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na wananchi kuvamia mipaka, mirathi, ununuzi wa maeneo kiholela, changamoto katika urasimishaji wa maeneo, utwaaji wa ardhi kwa manufaa ya umma, migogoro ya ndoa pamoja na ukosefu ama kupoteza nyaraka na kumbukumbu sahihi za umiliki wa ardhi.

“Ikitokea kifo cha mwenye ardhi bila kuacha miongozo mizuri ya ardhi kunaweza kusababisha ndugu kugombania ardhi au kutokukubaliana kuhusu usimamizi wa mali za marehemu ikiwemo ardhi, lakini pia unaweza kukuta eneo moja linaweza kutolewa au kutambuliwa na watu zaidi ya mmoja hivyo kusababisha migogoro katika umiliki’’ alifafanua Dkt. Homera. 

Aidha, Dkt. Homera ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari ili kupunguza migogoro ya ardhi kwa kutambua na kuthibitisha mipaka ya ardhi kabla ya kufanya muamala ama kutumia ardhi, kuhakikisha taarifa zinafahamika kwa wahusika, kufanya uhakiki kabla ya kufanya maamuzi ya ununuzi wa ardhi, kushirikisha viongozi na wataalam wa ardhi na inapohitajika wataalam wa sheria inapobidi, kuweka makubaliano maalum ya maandishi na maneno, kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu za umiliki wa ardhi pamoja na kupanga na kuandika mirathi mapema.

Dkt. Homera amesisitiza kuwa migogoro ya ardhi inapaswa kutatuliwa mapema na sio kuiacha ikue kwa kuwa kadri inavyokua inaongeza gharama za utatuzi pamoja na uhasama baina ya pande mbili.