ITUMIKIENI SERIKALI KWA UADILIFU NA WELEDI
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athuman Katimba (Mb.), ametoa wito kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuitumikia serikali kwa uadilifu na weledi pamoja na kuwa na moyo wa kutoa haki kwa wananchi wanaokwenda kuwahudumia.
Akizungumza wakati akifungua rasmi mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya 162 wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, jijini Arusha, 15 Aprili, 2026, Mhe. Katimba alisema hatua hii ya ajira na mafunzo inaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kutaka kuimarisha mfumo wa haki jinai nchini, na kuongeza kuwa ajira hizi zimekuja wakati ambao Mahakama za Mwanzo nchini zimeanza kupata Mahakimu wenye Shahada ya Kwanza ya Sheria, hivyo kuibua haja ya Mawakili wa Serikali kuwepo katika mahakama hizo ili kuendesha mashauri ya jinai na kuhakikisha haki inafika kwa kila mwananchi.
"Itumieni nafasi hii adimu kuitumikia Serikali kwa uadilifu, weledi na moyo wa kutoa haki kwa wananchi mtakaowahudumia," alisisitiza Mhe. Katimba.
Mapema akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Anthony Mwakitalu, alibainisha kuwa mafunzo hayo yanafanyika kwa lengo la kuwaandaa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuweza kufahamu maadili, taratibu na kanuni za utumishi wa umma, na kuongeza kuwa washiriki hao watafudishwa pia kuhusu masuala ya kifedha.
Mafunzo hayo yanafanyika jijini Arusha katika ukumbi wa Lush Garden Hotel na yanatarajiwa kutamatika Aprili 19, 2026.