JESHI LA MAGEREZA LINA UMUHIMU KATIKA KUHAKIKISHA WAFUNGWA WANAKUWA RAIA WEMA

Jeshi la Magereza nchini lina umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa haki jinai hususani katika kuwahifadhi, kuwarekebisha na kuwaandaa wafungwa ili warudi katika jamii wakiwa wamebadilika tayari na kuwa raia wema.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula aliyemuwakilisha Katibu Mkuu Eliakim Maswi, ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya Maafisa Sheria na Maafisa Urekebu 170 kutoka katika vituo mbalimbali vya magereza nchini.
Dkt Rwezimula amesema, mafunzo hayo yatawezesha maafisa hao kuwa na uelewa wa sheria mbalimbali zinazohusu haki za binadamu, uendeshaji wa magereza na mfumo wa haki jinai nchini.
“Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha kuwa maarifa, nyenzo na mbinu stahiki zinawafikia watendaji walio mstari wa mbele ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya Katiba na Haki”, amesisitiza Dkt. Rwezimula.
Ameongeza kuwa mafunzo haya pia yatawezesha maafisa hao kupata ujuzi na maarifa ya kukabiliana na changamoto za kiutendaji kama vile msongamano wa wafungwa, usalama wa magereza, urekebu wa wafungwa na pia kuepusha ukiukwaji wa haki za wafungwa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Wakili Jane Lyimo amesema awamu hii ya pili ya mafunzo haya ikikamilika jumla ya Maafisa Urekebu na Maafisa Sheria wa Jeshi la Magereza 290 watakua wamejengewa uwezo ambapo awamu hii ya pili ina Maafisa 170 na ile ya kwanza iliyofanyika mwezi Mei iliwafikia Maafisa 120.
Wakili Lyimo pia ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatarajiwa kukuza ushirikiano baina ya maafisa sheria na maafisa urekebu, kuwawezesha kuzingatia haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao hata katika mazingira magumu pamoja na kujenga mfumo wa haki unaotenda kazi kwa ufanisi, uwazi na kwa kutumia ushahidi wa kisheria.
Ameongeza kwa kuwasihi, “Ninyi mnatekeleza jukumu muhimu katika kubadilisha maisha ya watu waliokosea, kazi yenu sio tu kuwaweka ndani bali kuwawezesha kutoka wakiwa bora kwa kuwapa mafunzo, ushauri nasaha na mazingira ya kujirekebisha".
Kwa upande wake Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi la Magereza Nchini, CP. Nicodemus Tenga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwani imewezesha kupunguza mrundikano wa mahabusu na wafungwa magerezani.
“Kampeni hiyo iliyopewa jina la Mama Samia imewezesha wafungwa 12,000 kupata elimu na msaada wa kisheria huku mahabusu 6900 wakiachiwa kupitia msaada huo na hivyo kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa, awali mwaka 2021 wafungwa walikuwa 32,700 lakini takwimu za jana Juni 9, 2025 wamebaki wafungwa 26,896 pia uwiano wa wafungwa magarezani umekuwa asilimia 75 wafungwa na 25 mahabusu wakati zamani ilikuwa asilimia 50 wafungwa na 50 mahabusu.”, amefafanua CP Tenga.
Pia ameongeza kwa kumshukuru Rais Samia kwa kuunda Tume ya kutathmini mfumo wa haki jinai Nchini ambapo moja ya maelekezo ya timu hiyo ni kuwanoa maafisa na watendaji wa haki jinai ili wawe mahiri na hivyo kuwezesha kuandaliwa mafunzo hayo.