Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati Yapokea Taarifa ya Utendaji wa Wizara na Taasisi Zake

Imewekwa: 22 Aug, 2023
Kamati Yapokea Taarifa ya Utendaji wa Wizara na Taasisi Zake

Na George Mwakyembe, Emmanuel Msenga, WKS – Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepokea taarifa ya utendaji wa Wizara na Taasisi zake na kuipongeza Wizara namna inavyosimamia Taasisi zake katika kutekeleza majukumu yake ikisema kuwa taarifa inaonesha Wizara imekuwa na ushirikiano wa karibu na Taasisi zake katika kuhakikisha utendaji wa kazi unafanyika kwa weledi na kwa kushirikiana.

Akiongea kwenye kikao cha kupokea taarifa ya miezi mitatu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na Taasisi zake kwa kipindi cha miezi mitatu tarehe 22 Agosti, 2023 Jijini Dodoma Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama (MB) amesema “naipongeza Wizara kwa jitahada nzuri zinazofanywa kwa kusimamia Taasisi na kujenga ushirikiano ambao umekuwa na mafanikio katika majukumu yenu.”

Katika kikao hicho viongozi wa Taasisi wamewasilisha mafanikio yao na changamoto za Taasisi zao, Taasisi zilizowasilisha taarifa ya utendaji ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Serikali ya Mwendesha Mashtaka, Tume ya Kurekebisha Sheria pamoja na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambao wote walielezea mafanikio na changamoto zinazowakabili wakati wa utekelezaji wa majukumu. Moja ya changamoto ambayo imekuwa mtambuka kwa taasisi zote ni upungufu wa rasilimaliwatu.

Akijibu maswali yaliyoulizwa na wajumbe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema Wizara pamoja na Taasisi bado idadi ya watumishi haitoshi na majukumu yamekuwa mengi na watumishi wamekuwa wakijitoa kufanya kazi hadi muda wa ziada.

Aidha, mjumbe wa Kamati Mhe. Dkt Kaijage amezisisitiza Taasisi hizo kushughulikia masuala mbalimbali ya wafanyakazi wa Wizara na Taasisi hizo, ikiwemo upatikanaji wa makazi kwa wafanyakazi na kupandishwa vyeo wafanyakazi wenye sifa, “Kuna wafanyakazi ambao hawajapandishwa madaraja muda mrefu sana hao muwapandishe ili kuwapa morali na kazi,” alisema Mhe. Kaijage.

Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul, ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa pongezi pamoja na maoni ya kuhusu taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Taasisi hizo, na kuahidi kuendelea kushirikiana bega kwa bega na Taasisi hizo ili kuimarisha utendaji wake kwa manufaa ya nchi.

“Tukushukuru ndugu Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Kamati hii kwa maoni yenu, sisi kama Wizara pamoja na Taasisi zetu zote niwaahidi tutayafanyia kazi maoni haya, na kuongeza ushirikiano baina yetu ili kuboresha utendaji zaidi.” Alisema Mhe. Gekul.