KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA AWAMU YA PILI KUANZA 30 APRILI, 2026.
Wizara ya Katiba na Sheria inatarajia kuanza rasmi utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata haki bila ubaguzi ili kuweza kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma, tarehe 24 Aprili, 2026 wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainabu Athuman Katimba alisema kuwa Awamu ya Pili ya Kampeni hii inatarajiwa kuzinduliwa tarehe 30 Aprili 2026 katika mkoa wa Dodoma na kuendelea katika mikoa mingine kama ratiba itakavyokuwa.
‘’Naomba kuwataarifu waheshimiwa wabunge kuwa awamu ya pili ya utekelezaji wa Kampeni ya Msad awa Kisheria ya Mama Samia itazinduliwa rasmi tarehe 30 Aprili, 2026 jijini Dodoma, ambapo tunatarajia tutafika katika maeneo yote yenye uhitaji mkubwa hasa maeneo ya vijijini tofauti na kubakia kwenye miji’’ alisema Mhe. Katimba.
‘’Awamu hii wataalam wataweka kambi kwa siku kumi na tano katika kila halmashauri zote nchini ikilinghanishwa na siku kumi wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza lengo ikiwa ni kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika suala la upatikanaji wa haki’’ alisisitiza Mhe. Katimba.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ilianzishwa kwa maono ya Rais Mwenyewe, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nia ya kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa watanzania wote hususan wale wenye mahitaji maalum na wasioweza kumudu gharama za kuwa na uwakilishi unaimarishwa ambapo awamu ya kwanza ilitekelezwa katika kipindi cha kuanzia Machi 2023 hadi Juni, 2025 ambapo mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar ilifikiwa.