MABORESHO YA SEKTA YA SHERIA KUIMARISHA UTENDAJI WA SERIKALI
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainabu Athman Katimba amesema kuwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya sheria yanalenga kuifanya sekta hiyo kuchukua msimamo wa wazi na wa kimkakati utakaoisaidia kuwa muundombinu wa kitaifa katika uendeshaji wa shughuli za serikali katika ngazi zote.
Mhe. Katimba aliyasema hayo jijini Dodoma, 29 Aprili, 2026 alipokuwa akifunga rasmi kikao kazi cha mawakili wa serikali kilichofanyika kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yatakayoboresha utendaji kazi wao na hatimaye kuleta mabadiliko chanya kwa Taifa.
Mhe. Katimba alisema maboresho yaliyofanyika katika muundo mpya wa sekta ya sheria katika utumishi wa umma ambapo zimeongezwa kada kumi na moja kutoka kada moja iliyokuwepo awali ni hatua muhimu sana katika kukuza na kuimarisha sekta ya sheria nchini.
‘’Mmejadili kwa kina muundo mpya ulioboreshwa wa Sekta ya Sheria katika Utumishi wa Umma, maboresho haya yanalenga kuifanya Sekta hii kuwa sio tu sekta ya kutoa ushauri baada ya mambo kuharibika, bali kuchukua msimamo wa wazi na wa kimkakati wa kuifanya kuwa ni miundombinu ya kitaifa katika uendeshaji wa shughuli za serikali katika ngazi zote’’ alisema Mhe. Katimba.
Aidha Mhe. Katimba ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali kujiendeleza kitaaluma katika nyanja tofauti ili kujenga ubobezi mahsusi katika maeneo yao ya kazi hatua itakayowezesha kupatikana kwa wataalamu mahiri, waliobobea katika fani maalum jambo litakaloimarisha zaidi sekta ya sheria, kuifanya iheshimike na kuendelea kulinda hadhi yake kama taaluma adhimu (noble profession).
Kwa upande mwingine, Mhe. Katimba amewaelekeza mawakili wote wa Serikali kuanza kutekeleza mwongozo uliotolewa na Serikali unaowaruhusu kufanya kazi za kisheria za binafsi (private practice) pamoja na kuzingatia kikamilifu maadili ya utendaji wakati wa kutimiza wajibu wao.