MADEREVA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA WAHIMIZWA UADILIFU KAZINI

Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Fatma Kalovya amewahimiza madereva wa Wizara hiyo kuzingatia weledi ili kuendeleza ufanisi zaidi katika kazi zao.
Bi. Kalovya amesema hayo Mei 29, 2025 Mtumba Jijini Dodoma katika kikao kazi na madereva wa Wizara hiyo ambapo amewataka kujiepusha na mienendo mibaya ikiwemo matumizi ya vilevi wawapo kazini.
“Nyie ni watu muhimu sana katika utumishi bila nyie mambo mengi yatakwama hivyo nawasisitiza kwanza kuwa na nidhamu kazini lakini pia muwe na Upendo baina yenu na watumishi wote kwa ujumla”, amesema Kalovya.
Aidha amewasihi kuzingatia alama za barabarani ikiwemo kutokwenda mwendo kasi ili kujiepusha na ajali zinazosababishwa na mwendo kasi sambamba na kuwa washauri wazuri kwa viongozi wanao waendesha.
Kalovya pia amewasihi madereva hao kuzingatia utunzaji wa siri za Serikali na kuzingatia maadili ya uendeshaji wa Viongozi na Watumishi.