MATUMIZI YA TEHAMA KUIMARISHA SEKTA YA SHERIA
Serikali imejipanga kuimarisha sekta ya Sheria na haki kwa kupanua wigo wa Upatikanaji huduma kupitia uboreshaji wa matumizi ya TEHAMA, kuimarisha miundombinu ya mahakama na kuhakikisha mazingira rafiki yanayowawezesha wananchi kupata haki kwa wakati.
Hayo yamesemwa leo 25 Februari, 2026 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba alipofanya ziara ya kikazi katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia cha Mahakama ya Tanzania kilichopo Temeke, jijini Dar Es Salaam.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Katimba amesema Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha sekta ya sheria na haki kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma kwa kuboresha matumizi ya TEHAMA, kuimarisha miundombinu ya mahakama, na kuweka mazingira rafiki yatakayorahisisha wananchi kupata haki kwa wakati.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki bila vikwazo, kwa wakati na katika mazingira yanayozingatia weledi na utu,” amesema Mhe. Katimba.
Kwa upande wake Mchungaji Daud Mashimo, mmoja wa wananchi waliopata huduma katika kituo hicho amepongeza ubora wa huduma zinazotolewa akieleza kuwa kituo hicho ni mfano wa kuigwa kutokana na uratibu mzuri na mazingira rafiki kwa wateja.
Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia cha Temeke kinajumuisha Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Watoto na Mahakama Kuu na kinatoa huduma mbalimbali ikiwemo msaada wa kisheria, ushauri nasaha pamoja na chumba maalum cha huduma za kunyonyesha, hatua inayolenga kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote kwa kuzingatia mahitaji maalum ya makundi tofauti katika jamii.
Ziara ya Naibu Waziri ililenga kukagua utendaji kazi wa kituo hicho, ubora wa huduma zinazotolewa, pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa haraka, kwa usawa na kwa kuzingatia utu.