MWENGE WA UHURU WAANGAZIA UTOAJI HAKI KWA WANANCHI RUVUMA

Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, ametoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kupata huduma ya msaada wa kisheria, hususani wale wanaokumbwa na changamoto mbalimbali za kisheria.
Ametoa wito huo Mei 14, 2025, wakati wa uzinduzi wa miradi iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Songea.
Mhe. Ndumbaro amesema huduma hiyo itatolewa katika viwanja vya Kata ya Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) ambayo inalenga kuyafikia makundi ya wananchi waliokosa uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria na kuwapatia msaada wa kitaalamu bure.
Ameeleza kuwa wananchi watakaofika kwenye eneo hilo watapata huduma za kisheria zinazohusu masuala ya ndoa, mirathi, madai, migogoro ya ardhi, pamoja na matatizo mengine ya kisheria yanayowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Huduma hizo zitatolewa na Wanasheria waliobobea na Watumishi wa Serikali waliobobea katika masuala ya sheria.
Mhe. Ndumbaro amewahimiza wananchi wa Songea kutumia fursa hiyo kupata Haki zao kwa njia halali na kuimarisha utawala wa Sheria katika jamii.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mkazo katika kuwahudumia wananchi kwa ukaribu na kwa vitendo.