Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TANZANIA, JAPAN KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA SHERIA

Imewekwa: 15 Sep, 2026
TANZANIA, JAPAN KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA SHERIA

Serikali ya Tanzania imesema ipo tayari kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Japan katika sekta ya sheria, hususan katika kujenga uwezo wa wataalamu wa sheria, kubadilishana uzoefu na kuimarisha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi Baraka Luvanda, wakati wa mazungumzo na ujumbe wa Serikali ya Japan ulioongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Pili ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan, Bw. Hironori Suzuki,akiwa ameambatana  na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yoichi Mikami, katika kikao kilichofanyika tarehe 14 Septemba 2026 katika Ukumbi wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mtumba jijini Dodoma.

Balozi Luvanda amesema maeneo yanayopendekezwa katika ushirikiano huo ni pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu wa sheria, kubadilishana uzoefu na mbinu bora, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kisheria, pamoja na kuimarisha Kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC), ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa magari maalumu na vifaa vya kidijitali.

Aidha, Tanzania imependekeza kushirikiana na Japan katika kufanya tafiti linganishi za kisheria, kubadilishana utaalamu na uzoefu, pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali katika sekta ya sheria.

Kwa upande wake, Balozi Mikami ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada inazozifanya katika kuimarisha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi. Amesema Japan ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta ya sheria, kwa kuangalia na kuweka kipaumbele katika maeneo ya kimkakati yaliyowasilishwa na Tanzania.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuchangia katika kuimarisha upatikanaji wa haki, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.