Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TANZANIA YAWEKA WAZI MAFANIKIO YA MSAADA WA KISHERIA, SHERIA 446 ZATAFSIRIWA KWA KISWAHILI

Imewekwa: 13 Nov, 2026
TANZANIA YAWEKA WAZI MAFANIKIO YA MSAADA WA KISHERIA, SHERIA 446 ZATAFSIRIWA KWA KISWAHILI

Tanzania imeweka wazi mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi, ikiwemo kutafsiri sheria kuu 446 kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili na kuwafikia wananchi 7,885,295 kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Mafanikio hayo yameelezwa leo Novemba 12, 2026 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athuman Katimba (Mb.), alipowasilisha uzoefu wa Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Upatikanaji wa Haki unaofanyika Sun City, Afrika Kusini, chini ya ajenda ya “Kuimarisha Mifumo ya Haki Inayomlenga Mwananchi: Maendeleo na Mafanikio”.

Akieleza kuhusu tafsiri ya sheria hizo, Mhe. Katimba amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kuelewa sheria na haki zao kwa kutumia lugha ya Kiswahili, hivyo kuziba pengo kati ya sheria na wananchi inaowahudumia. Ameongeza kuwa sheria hizo zimewekwa wazi ili wananchi waweze kuzifikia, kuzielewa na kuzitumia.

Aidha, amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, iliyozinduliwa mwaka 2023, imefikia watu 7,885,295, wakiwemo wanawake 4,060,286 na wanaume 3,825,009. Kupitia kampeni hiyo, wafungwa 19,511 wamepatiwa elimu ya sheria, wafungwa 3,849 wamepata msaada wa kisheria, huku malalamiko 1,239 yakisaidiwa kutatuliwa.

Katika mkutano huo, Mhe. Katimba amefikisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuipongeza Serikali ya Afrika Kusini kwa kuandaa mkutano huo unaofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Katiba ya nchi hiyo. Amesema Tanzania inatambua upatikanaji wa haki kama haki ya msingi ya binadamu na nguzo ya maendeleo endelevu, huku ikiendelea kutekeleza Lengo la 16 la Maendeleo Endelevu (SDG 16).

Akihitimisha, Mhe. Katimba amesema Tanzania itaendelea kuimarisha utawala wa sheria na mifumo ya haki inayomlenga mwananchi bila kujali hali yake ya kijamii au kiuchumi. Aidha, ameeleza utayari wa Tanzania kuendeleza ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kujenga ubia wa kimkakati na Afrika Kusini pamoja na nchi nyingine shiriki.