TANZANIA IMEPIGA HATUA ULINZI WA HAKI ZA BINADAMU-MHE. KATIMBA
Tanzania imeendelea kupiga hatua katika kukuza, kulinda na kuendeleza haki za binadamu katika sekta mbalimbali, hatua ambayo imechangiwa na utekelezaji wa mapendekezo yaliyokubaliwa kimataifa pamoja na juhudi za ndani za serikali.
Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, ameyasema hayo leo 27 Aprili, 2026 mkoani Morogoro, wakati akifungua rasmi kikao kazi cha uhakiki na uthibitishaji wa Rasimu ya Taarifa ya Hali ya Haki za Binadamu katika mzunguko wa nne wa Mfumo wa Mapitio ya Kipindi Maalum (UPR), ambapo amebainisha kuwa mafanikio hayo yamekuwa chachu ya kuimarisha amani, mshikamano na utulivu nchini.
Mhe. Katimba amesisitiza kuwa Tanzania imekuwa ikitekeleza kwa vitendo wajibu wake wa kulinda haki za msingi za binadamu kwa kuzingatia misingi ya sheria, sera na mikakati mbalimbali inayolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata haki zake stahiki bila ubaguzi.
Aidha, ameongeza kuwa Tanzania imekubali kutekeleza jumla ya mapendekezo 187 yaliyotokana na ahadi ya kitaifa iliyowasilishwa mbele ya jumuiya ya kimataifa, akieleza kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo ni muhimu katika kuimarisha ustawi wa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Mhe. Katimba pia amewahimiza wataalamu wanaoshiriki kikao hicho kuhakikisha wanaandaa taarifa yenye ubora, inayojikita katika kuonesha mabadiliko halisi yaliyopatikana, pamoja na kuwasilisha takwimu sahihi na zenye kuaminika kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Haki za Binadamu, Bw. Richard Kilanga, amesema kuwa lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuhakiki na kuthibitisha rasimu ya taarifa ya hali ya haki za binadamu ili kuhakikisha inakuwa sahihi, kamilifu na inayoakisi hali halisi ya utekelezaji wa haki hizo nchini.
Amebainisha kuwa kikao hicho kinatoa fursa kwa wadau mbalimbali kuchangia maoni yao, kuboresha taarifa hiyo na kuhakikisha inakidhi viwango vinavyotakiwa kimataifa kabla ya kuwasilishwa rasmi.