TANZANIA YAIMARISHA ULINZI WA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU
Serikali ya Tanzania inaendelea kuimarisha juhudi za kulinda, kukuza na kutetea haki za watu wenye ulemavu kupitia utekelezaji wa sera, sheria na mikakati mbalimbali inayolenga kuhakikisha kundi hilo linapata fursa sawa na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Rwezimula, wakati akifungua kikao cha kuhakiki na kuhuisha Rasimu ya Taarifa ya Nchi ya Utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) kilichofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Morena jijini Dodoma tarehe 08 Juni, 2026.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Rwezimula amesema kuwa Tanzania iliridhia Mkataba wa CRPD tarehe 10 Novemba mwaka 2009 ikiwa na dhamira ya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanatambuliwa kikamilifu kama sehemu muhimu ya jamii, kwa kuondoa vikwazo vinavyowakabili na kuwapatia haki, fursa na huduma kwa usawa bila ubaguzi wa aina yoyote.
Ameeleza kuwa tangu kuridhiwa kwa mkataba huo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria na kisera ili kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu, hatua ambazo zimejengwa juu ya msingi wa Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na Sera ya Watu Wenye Ulemavu ya Zanzibar ya mwaka 2018.
Dkt. Rwezimula amebainisha kuwa utekelezaji wa mkataba huo umeungwa mkono pia na uwepo wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Sura ya 183 kwa Tanzania Bara pamoja na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 8 ya Mwaka 2022 ya Zanzibar, ambazo zimeweka msingi imara wa kulinda na kukuza haki za watu wenye ulemavu pamoja na kuimarisha ushiriki wao katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Aidha, amesema kuwa zoezi la kuhakiki na kuhuisha Rasimu ya taarifa ya utekelezaji wa CRPD ni muhimu kwa kuwa linatoa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati madhubuti ya kuendelea kuboresha mazingira ya watu wenye ulemavu nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Haki za Binadamu Kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Beatrice Mpembo amewataka washiriki wa kikao hicho kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wa masuala ya watu wenye ulemavu kutumia nafasi hiyo kutoa michango yenye kujenga na Taarifa sahihi zitakazosaidia kuandaa ripoti yenye ubora na inayoakisi maendeleo ya Taifa.
Bi. Mpembo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa kwa vitendo, na kuonesha ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa kwani ni nguzo muhimu ya kujenga jamii jumuishi, yenye usawa na inayotoa fursa kwa kila mwananchi bila kuachwa nyuma.