Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tume ya Kurekebisha Sheria Jitangazeni Wadau wa Sheria Wawatambue - N/W Sagini

Imewekwa: 09 May, 2024
Tume ya Kurekebisha Sheria Jitangazeni Wadau wa Sheria Wawatambue - N/W Sagini

Na Yasinta Kissima – WKS Dodoma

Akizungumza mara baada ya kutembelea Makao Makuu ya Tume ya Kurekebisha Sheria na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini Dodoma, Mei 8, 2024 Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria kujitangaza na kutoa elimu kwa Wadau wa Sheria ili Tume iweze kushiriki ipasavyo katika kufanya mapitio ya Sheria mbalimbali.

Mhe. Sagini amesema kuwa ipo changamoto ya baadhi ya Wadau wa Sheria kutokujua vizuri majukumu ya Tume na hivyo kuchelewa kuishirikisha Tume katika kufanya mapitio ya Sheria zao.

"Tume ipo kwa mujibu wa Sheria na Katiba yetu na inawajibu wa kufanya tathmini ya Sheria zilizopo kuona zile zilizopitwa na wakati, zinazohitaji marekebisho, utekelezaji wake na changamoto ili kuishauri Serikali namna bora ya kuboresha Sheria hizo." Alisema Naibu Waziri Sagini.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya Maendeleo, Mhe. sagini amesema kuwa mpaka sasa Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo chini yake imeanza kuandika maandiko mbalimbali ili kuweza kuvutia fedha kutoka Serikali au Wadau mbalimbali wa Maendeleo na ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria kushiriki ipasavyo na kutoa mapendekezo yao katika miradi itakayopendekezwa.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu amesema kwa kuwa Tafiti za Kisheria ni sehemu mojawapo ya majukumu ya Tume, ni vyema wakaanzisha mashirikiano na Vyuo mbalimbali vya Elimu ya Juu vyenye kada za Kisheria ili kufanya tafiti nyingi na kupata maarifa zaidi.