Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ULEGA AITAKA IJA KUIMARISHA NIDHAMU, MAADILI NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA MAFUNZO

Imewekwa: 23 Nov, 2026
ULEGA AITAKA IJA KUIMARISHA NIDHAMU, MAADILI NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA MAFUNZO

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb.), ameitaka Menejimenti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kuendelea kusimamia nidhamu, maadili na uadilifu kwa wanachuo, akisisitiza kuwa chuo hicho kina jukumu muhimu la kuandaa viongozi na wataalamu wa sekta ya sheria na umma.

Akizungumza Novemba 21, 2026, katika kikao chake na Menejimenti ya Chuo hicho, Mhe. Ulega amesema IJA ni taasisi inayozalisha mahakimu, majaji, watendaji wa Serikali na viongozi mbalimbali, hivyo ni muhimu kuhakikisha wahitimu wanakuwa na nidhamu, uadilifu na mienendo inayozingatia mila na desturi za taifa.

Aidha, Waziri Ulega ameitaka menejimenti kuongeza msisitizo katika matumizi ya teknolojia ili kuwajengea wanachuo uwezo zaidi na kuwafanya kuwa mahiri katika matumizi ya teknolojia yanayoendelea kubadilisha mifumo ya utendaji kazi duniani.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ulega ameipongeza menejimenti kwa mazingira mazuri na yanayovutia ya chuo hicho, huku akihimiza kuendeleza juhudi za utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti, kutunza bustani na kuhakikisha programu za uhifadhi wa mazingira zinaendelea kutekelezwa bila kusuasua.

Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unapaswa kuwa endelevu ili kuendelea kukifanya chuo hicho kuwa sehemu safi, yenye kuvutia na inayowezesha ufundishaji na ujifunzaji katika mazingira bora.