UTUNGAJI WA SHERIA NI ZOEZI LA KISERA LINALOANDALIWA KITAALAM

Naibu Katibu Mkuu,Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula ametoa rai kwa washiriki wa kikao kazi cha kupitia Rasimu ya Muswada wa marekebisho ya Sheria za Haki Jinai kuzingatia malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha kuwa Haki jinai inapatikana kwa wote.
Naibu Katibu Mkuu Katiba na Sheria ameyasema hayo Mei 14, 2025 wakati akifungua kikao kazi Cha kupitia Rasimu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Haki Jinai (The Criminal Laws-Miscelkenious Amendment Bill 2025).
Dkt. Rwezimula alisema kuwa utungwaji wa Sheria ni zoezi la kisera linaloandaliwa kitaalam ambapo Bunge ndio chombo pekee chenye mamlaka ya kuamua muswada husika kuwa Sheria.
Alisema kuwa, Wizara ya Katiba na Sheria ilipewa majukumu ya kufanya maboresho ya vifungu vya sheria vilivyobainika kuwa na changamoto wakati wa utekelezaji wake kwa kuwa Wizara imepewa Hati Idhini ya kusimamia Masuala ya Haki na Sheria zote nchini.
Alifafanua kuwa, Marekebisho ya Sheria ya Haki jinai ni miongoni mwa maboresho yanayoendelea kusimamiwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Sheria na Haki.
“Mtakumbuka Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alipoingia madarakani alikuja na falsafa ya R nne, Moja ya R hizo ni maboresho katika Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Sheria na Haki ” alisema.
Aidha, Dkt. Rwezimula amewapongeza wataalam wa Idara ya Sheria wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kusimamia na kuratibu maandalizi ya Muswada huo ambao ni sehemu ya maboresho katika Sekta ya Haki Jinai.