Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WANANCHI MILIONI KUMI WAPATIWA MSAADA WA KISHERIA DKT NDUMBARO

Imewekwa: 16 Jun, 2025
WANANCHI MILIONI KUMI WAPATIWA MSAADA WA KISHERIA DKT NDUMBARO

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro amesema hadi kufikia mwezi Juni, 2025, jumla ya wananchi 10,827,811 ikijumuisha wanawake 5,844,025 wanaume 4,983,786 wamepatiwa huduma za msaada wa kisheria ikiwemo elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala. 

Dkt Ndumbaro ameyasema hayo leo Juni 16 2025 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Mkoani Dar Es Salaam ambapo ameongeza kuwa wananchi hao wamepata Msaada wa Kisheria kupitia madawati ya Msaada wa Kisheria yaliyo anzishwa kwa ngazi za halmashauri huku akiongeza kuwa jumla ya migogoro 27,138 ilipokelewa na kufanyiwa kazi.

Pia ameeleza kuwa Jumla ya wafungwa na mahabusi 8,544 walipata huduma za msaada wa kisheria.kati yao 601 walipata dhamana na kuachiliwa na 1,078 walipata ushauri wa kisheria huku akimuomba Waziri Mkuu akabidhi seti 30 ya vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kuwezesha mahakama mtandao.

"Tumekwenda mpaka kwenye Magereza, tumetoa msaada wa kisheria kwa wafungwa 28,137 na leo Mhe. Mgeni rasmi tutakuomba ukabidhi vifaa kwaajili ya magereza, vifaa vya TEHAMA ambavyo vitafanya wafungwa na mahabusu waweze kusikiliza na kuendesha kesi zao wakiwa Magerezani na hivyo kupunguza gharama za usafiri kwenda Magereza na kurudi, kupunguza kuahirishwa kwa kesi kutokana na kukosekana kwa usafiri lakini pia kufanya Magereza yawe sehemu salama zaidi.", amesisitiza Dkt. Ndumbaro.