Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WATUMISHI WAPYA NPS WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Imewekwa: 21 Apr, 2026
WATUMISHI WAPYA NPS WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Homera amewataka watumishi wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kuzingatia maadili, weledi na misingi ya utumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Dkt. Homera amesema hayo Aprili, 19, 2026 Jijini Arusha wakati akifunga mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa NPS na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Serikali sambamba na kutunza siri za Serikali na kuwajibika ipasavyo katika nafasi walizopewa.

Amesema Serikali ina matarajio makubwa kwa watumishi hao katika kuimarisha utoaji wa haki jinai nchini kupitia majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano, ubunifu na nidhamu.

"Nina imani mafunzo haya yamewajengea uwezo wa kutosha kwenda kutekeleza majukumu yenu kwa bidii, weledi na kwa kuzingatia misingi ya haki na utumishi wa umma," amesema Dkt. Homera.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha taasisi za haki jinai kwa kuongeza nguvu kazi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Bw. Sylvester Mwakitalu amesema baada ya mafunzo ya siku tano yaliyohusu majukumu ya kazi, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, waajiriwa hao wako tayari kwenda kutoa huduma za kimashtaka kwa jamii kwa weledi na ufanisi.

DPP Mwakitalu ameeleza kuwa mafunzo hayo yalijumuisha watumishi wapya 162 wakiwemo Mawakili wa Serikali, Makatibu sheria, Madereva, Wahasibu, Wasaidizi wa hesabu, Watakwimu, Maafisa Tehama, Watunza kumbukumbu, Waandishi waendesha ofisi  na Afisa habari.