Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA, UNDP WADHAMIRIA KUPELEKA HAKI KWA WANANCHI

Imewekwa: 16 Apr, 2026
WIZARA, UNDP WADHAMIRIA KUPELEKA HAKI KWA WANANCHI

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (Mb) amekabidhi magari na vifaa vya TEHAMA kwa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na kasi katika upatikanaji wa Haki kwa wananchi. 

Akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika Aprili 15, 2026 Mtumba Jijini Dodoma Mhe. Homera amesema kuwa kukabidhiwa kwa magari 5 na Kompyuta mpakato 180 ni hatua muhimu katika kuimarisha mifumo ya kidijitali ndani ya Mahakama na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora 

“Upatikanaji wa vifaa hivi utawezesha sekta ya sheria kutekeleza majukumu na kuleta matokeo chanya na kutekeleza Dira 2050 inayolenga kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi na linalozingatia misingi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kuimarisha mifumo ya utoaji Haki” amesema Dkt. Homera.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma za kisheria kwa njia rahisi na kwa wakati kufuatia upatikanaji wa magari hayo.

Katika hatua nyingine Mhe. Homera ameshukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji haki nchini na kuwezesha kutolewa kwa vitendea kazi hivyi chini ya Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Awali akitoa salamu za wizara Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula amesema kuwa wizara inaendelea kujenga na kuimarisha mifumo jumuishi itakayowezesha taasisi mbalimbali kushirikiana kwa ufanisi, kubadilishana taarifa kwa wakati na kutoa  huduma zilizounganishwa kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwakilishi  Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP Bw. Shigeki Komatsubara amesema  kuwa upatikanaji wa vifaa hivyo utarahisisha uandishi wa nyaraka za kisheria, kulinda taarifa muhimu, hivyo kujenga mfumo wa haki ulio jumuishi na unaofikika kwa wananchi kwa urahisi.

Katika makabidhiano hayo Mahakama ya Tanzania imepokea Kompyuta mpakato 150 na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepokea Magari 5 na Kompyuta mpakato 30