WIZARA YA KATIBA YAWAPONGEZA WALIOFUATA MARIDHIANO KUMALIZA MIGOGORO
Wizara ya Katiba na Sheria imewatambua na kuwapongeza baadhi ya wanufaika wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa kuchagua njia ya maridhiano katika kutatua migogoro yao.
Miongoni mwa wanufaika hao ni Bw. Abel Ndelengo ambaye kwa takribani miaka 15 alikuwa na mgogoro wa shamba la korosho lenye ukubwa wa ekari nane na Bi. Frola Mkondya ambapo mgogoro huo ulitokana na mauziano ya shamba hilo alilonunua kutoka kwa familia ya muuzaji mwaka 2011 kwa shilingi milioni moja na elfu hamsini.
Akizungumza na wanufaika hao, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amewapongeza kwa kukubali kumaliza migogoro yao kwa njia ya maridhiano, akisema hatua hiyo inasaidia kudumisha amani na mshikamano katika jamii.
Amesema migogoro ya muda mrefu huathiri ustawi wa watu na kuzuia maendeleo, hivyo ni muhimu wananchi kuchagua njia za amani katika kutatua tofauti zao.
Katika kutambua uamuzi wa Bw. Ndelengo kukubali kuachia shamba hilo kwa maridhiano, Wizara imemzawadia kiasi cha shilingi milioni 15 kama pongezi kwa uzalendo na mchango wake katika kudumisha amani.
Kwa upande wake, Bw. Ndelengo amesema ameridhishwa na namna suala lake lilivyopatiwa ufumbuzi kupitia kampeni hiyo, na kwamba alikubali kurejeshewa fedha alizolipa aliponunua shamba hilo ili kumaliza mgogoro na kuendelea kuishi kwa amani.
Serikali inaeendelea kutoa wito kwa wananchi kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro ili kudumisha amani na mshikamano ndani ya familia na jamii kwa ujumla.