TAARIFA KWA UMMA: UWASILISHAJI WA TAARIFA KWENYE MFUMO WA NaLIS
TAARIFA KWA UMMA
Wizara ya Katiba na Sheria inawataarifu watoa huduma wote wa Usuluhishi, Upatanishi, Uendeshaji wa Maridhiano na Majadiliano waliosajiliwa na wale ambao wana nia ya kuwa watoa huduma hizo, kuwa Wizara kupitia Kitengo cha Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala inapenda kuwafahamisha kuwa katika kufanya maboresho ya Mfumo, taarifa za usajili zimehamishwa (migrated) kutoka mfumo wa zamani https://tlegalaid.sheria.go.tz kwenda kwenye Mfumo mpya wa NaLIS (https://nalis.sheria.go.tz)
Na kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Sura ya 33 na Kanuni za Uthibitishaji wa Watoa Huduma za Maridhiano, Majadiliano, Upatanishi na Usuluhishi, 2021(Reconciliation, Negotiation, Mediation and Arbitration (Practitioners Accreditation) Regulations, 2021), kila mtoa huduma anayetoa huduma tajwa hapo juu anatakiwa awe amesajiliwa na kuwa na cheti halali wakati wote anapotekeleza majukumu yake.
Ili kuendelea kupata huduma bila usumbufu ikiwa ni pamoja na kuwasilisha maombi ya uhuishaji wa cheti (renewal), kufuatilia hali ya maombi, na huduma nyingine muhimu, kwa majina yaliyoainishwa katika SEHEMU A ya tangazo hili, mnaombwa kuingia kwenye mfumo mpya kupitia https://nalis.sheria.go.tz na kuhuisha taarifa. Mwongozo wa haraka unaoonyesha hatua rahisi za kufuata ili kukamilisha uhuishaji huu umetumwa kwenye barua pepe zenu, na pia ujumbe mfupi (SMS) umetumwa kwenye namba zenu za simu ukionesha barua pepe iliyotumika.
Aidha, kwa wale ambao majina yao yameainishwa katika SEHEMU B ya tangazo hili, mnaombwa kuwasilisha taarifa zifuatazo: (i) kwa mtoa huduma binafsi: majina kamili, namba ya NIDA, Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), uraia, tarehe ya kuzaliwa, anuani, mkoa, barua pepe, namba ya simu, jinsia, tarehe ya usajili na tarehe ya cheti kuisha muda (kwa waliosajiliwa), pamoja na namba ya cheti; na (ii) kwa taasisi: taarifa za taasisi (jina, TIN, barua pepe, namba ya simu, anuani, mkoa na maelezo ya huduma zinazotolewa na namba ya cheti) pamoja na taarifa za mtu wa mawasiliano (focal person) kama zilivyoainishwa katika kipengele (i). Taarifa hizi zitumwe kupitia barua pepe support.nalis@sheria.go.tz.
Wizara inatoa wito kwa watoa huduma wote kuzingatia kikamilifu tangazo hili pamoja na Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia taaluma za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ili kulinda uadilifu wa huduma, maslahi ya wadau pamoja na kuimarisha imani ya umma. Kwa mawasiliano zaidi, wasiliana nasi kupitia support.nalis@sheria.go.tz au Piga 0762 014 029 / 0719 496 957.
Mwisho wa uwasilishaji wa taarifa hizi ni tarehe 30 Oktoba, 2026.
Imetolewa na:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
25 SEPTEMBA, 2026